Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeitaka sekta binafsi kujitokeza kwa wingi kuwekeza na kushiriki katika biashara ya kaboni, ikieleza fursa zilizopo katika sekta hiyo zinaweza kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza mapato ya nchi na kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha sekta binafsi inakuwa mshirika muhimu katika safari ya kuelekea uchumi wa kijani, huku ikichangia maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi.
Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili zikiwemo misitu, ardhi, maeneo oevu na bahari, ambazo zinaifanya nchi kuwa na nafasi kubwa katika uzalishaji wa mikopo ya kaboni inayotambulika kimataifa.
Msisitizo huo umetolewa leo Jumatano, Desemba 17, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Profesa Peter Msoffe wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau wa mazingira kujadili ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa 30 wa mabadiliko ya tabianchi (COP 30) nchini Brazil.
Profesa Msoffe amesema kupitia mkutano huo Tanzania imeendelea kuona kuwa kuna fursa kubwa kwenye biashara ya kaboni na sekta binafsi inaweza kuwa na mchango kwa kuweka bunifu mbalimbali za kuyafikia masoko ya biashara hiyo.
“Serikali imeeleza tayari imeweka mifumo na miongozo inayotoa uhakika kwa wawekezaji, ikiwemo mfumo wa usajili wa miradi ya kaboni, utaratibu wa ugawaji wa mapato pamoja na usimamizi wa miradi ili kuhakikisha faida zinawanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Hatua hizo zinalenga kuondoa hofu na sintofahamu ambazo hapo awali zilifanya baadhi ya wawekezaji na kampuni binafsi kusita kuingia kwenye sekta hiyo, bado tunasisitiza tunahitaji zaidi sekta binafsi iichangamkie fursa hii,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo amesema biashara ya kaboni siyo tu fursa ya kimazingira bali pia ni chanzo kipya cha mapato kwa sekta binafsi, hasa kwa kampuni zinazojihusisha na uhifadhi wa misitu, kilimo endelevu, nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira.
Naibu katibu mkuu huyo amebainisha Serikali iko tayari kushirikiana na wawekezaji binafsi kuendeleza miradi itakayokidhi vigezo vya soko la kimataifa la kaboni.
Mbali na hilo, Profesa Msoffe amezitaka wizara na taasisi za Serikali zinahusika na masuala ya mazingira kuandaa miradi ya kimkakati itakayoweza kufadhiliwa chini ya utekelezaji wa Dira 2050 na maamuzi ya COP30.
Ametaja maeneo yatakayopewa kipaumbele ni miradi ya uhimilivu, mifumo ya tahadhari mapema, matumizi ya nishati safi ya kupikia na teknolojia, biashara ya kaboni na uhifadhi na usimamizi wa misitu, maji, kilimo na taka.
Kwa upande wake, Mshauri wa Rais Mazingira- Mabadiliko ya Tabianchi, Dk Richard Muyungi amesema ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano huo umekuwa na manufaa makubwa si tu kwa kujifunza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi bali kupata ahadi za ushirikiano na ufadhili wa Dola za Marekani milioni 447.12 na Euro 500,000.
Dk Muyungi ambaye katika mkutano huo alikuwa pia Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) amesema nafasi hiyo imeifanya nchi kuimarisha hadhi yake kimataifa.
“Kupitia nafasi hiyo Tanzania imewezesha kujadiliwa na kukubalika kwa ajenda ya Nishati Safi ya kupikia, kukubalika kwa hoja ya upatikanaji wa umeme wa bei nafuu kwa watu wote,” amesema.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Kamisha wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Rished Beda amesema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa kukabiliana na athari za mazingira na mabadiliko ya tabianchi kiasi cha Sh2 trilioni kimepatikana.