Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuanzishwa kwa mzingiro kamili na wa jumla dhidi ya meli zote za mafuta zilizo chini ya vikwazo, zinazoingia au kutoka nchini Venezuela.
Kupitia ujumbe alioutoa kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema serikali ya Rais Nicolás Maduro imetangazwa kuwa shirika la kigaidi la kigeni, akiituhumu kwa kuiba mali za Marekani pamoja na kujihusisha na ugaidi, biashara ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu.
“Kwa msingi huo, leo ninaamuru mzingiro kamili na wa jumla wa meli zote za mafuta zilizo chini ya vikwazo zinazoingia na kutoka Venezuela,” aliandika Trump.
Tamko hilo linakuja wiki moja baada ya Marekani kukamata meli ya mafuta karibu na pwani ya Venezuela.
Serikali ya Caracas ilijibu kwa kukataa vikali hatua hiyo, ikiitaja kuwa tishio lisilokubalika na la kichokozi.
Katika ujumbe wake, Trump alidai Venezuela “imezungukwa kikamilifu na msafara mkubwa zaidi wa kijeshi kuwahi kukusanywa katika historia ya Amerika Kusini”, akisisitiza kuwa nguvu hiyo itaendelea kuongezwa na kwamba itakuwa hali ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Trump pia aliishutumu serikali ya Maduro kwa kutumia mapato ya mafuta yaliyoibwa kufadhili shughuli za uhalifu ikiwemo ugaidi wa dawa za kulevya, biashara ya binadamu, mauaji na utekaji nyara.
Utawala wa Trump umekuwa ukiishutumu Venezuela mara kwa mara kwa kuhusika katika usafirishaji wa dawa za kulevya.
Tangu Mwezi Septemba, jeshi la Marekani limesema limeua takribani watu 90 katika mashambulizi dhidi ya boti lilizodai zilikuwa zikisafirisha fentanyl na dawa nyingine haramu kuelekea Marekani.
Katika miezi ya karibuni, Marekani pia imeongeza uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo kwa kupeleka meli za kivita.
Venezuela, ambayo ni miongoni mwa nchi zenye akiba kubwa zaidi ya mafuta duniani, imekuwa ikiituhumu Washington kwa nia ya kunyakua rasilimali zake.
Marekani, chini ya tawala za Trump na rais wa zamani Joe Biden, imekuwa ikiipinga serikali ya Maduro kwa muda mrefu, ikiweka vikwazo vikali kama sehemu ya juhudi za kumlazimisha aondoke madarakani.
Wiki iliyopita, Washington iliweka vikwazo vipya dhidi ya meli sita zaidi ilizosema zilikuwa zikisafirisha mafuta ya Venezuela. Hatua hizo pia ziliwalenga baadhi ya ndugu wa Rais Maduro pamoja na kampuni zinazohusishwa na kile Marekani inachokiita serikali haramu.
Siku moja kabla, Ikulu ya Marekani ilitangaza kukamatwa kwa meli ya mafuta iitwayo Skipper karibu na pwani ya Venezuela, ikidai ilihusika katika usafirishaji haramu wa mafuta na kwamba ingetolewa hadi bandari ya Marekani.
Serikali ya Venezuela ililaani vikali kukamatwa kwa meli hiyo, huku Rais Maduro akidai Marekani “iliwateka nyara wafanyakazi wa meli” na “kuiba chombo hicho”.
Kabla ya oparesheni hiyo, Marekani ilikuwa imeongeza kwa kiasi kikubwa uwepo wake wa kijeshi katika Bahari ya Caribbean, ikihusisha maelfu ya wanajeshi pamoja na manowari kubwa zaidi duniani, USS Gerald Ford, iliyowekwa katika eneo la karibu na Venezuela.
Mbunge wa Marekani kutoka Texas, Joaquin Castro wa Chama cha Democratic, alisema mzingiro wa majini uliotangazwa na Trump “ni kitendo cha vita kisicho na shaka”. Aliongeza kuwa Bunge la Marekani linatarajiwa kupiga kura juu ya azimio litakalomuelekeza rais kusitisha uhasama dhidi ya Venezuela.