Dar es Salaam. Safari ya vyama vya upinzani barani Afrika katika kuisaka dola inaendelea kuwa ngumu na yenye miiba, huku vikwazo vya kisiasa, kisheria na kiusalama vikizidi kutishia uhai na mustakabali wa viongozi wake.

Licha ya kuanzishwa kwa vyama vya upinzani kwa dhamira ya kuimarisha demokrasia, kutoa mbadala wa sera na kuikosoa serikali kwa uwajibikaji, uhalisia umekuwa tofauti na matarajio.

Katika nchi nyingi, upinzani unatarajiwa kuwa nguzo ya kulinda haki za raia, kusimamia uchaguzi huru, kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha mabadiliko ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia.

Hata hivyo, hali halisi uwanjani inaonyesha taswira tofauti kabisa inayoonesha mazingira yasiyo rafiki kwa vyama hivyo. Mara kwa mara mikutano ya kisiasa huzuiwa kwa madai ya kiusalama.

Pia viongozi wake hukamatwa, kuwekwa vizuizini hatua zinazodhoofisha uwezo wao wa kushiriki kikamilifu katika siasa.

Katika mataifa mengi ya Afrika, upinzani umegeuzwa kuwa tishio linalopaswa kuzimwa badala ya kuwa mshirika wa maendeleo.

Wachambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa wanasema siasa za upinzani ni sawa na kuweka rehani mustakabali wa nchi na hata viongozi wake kutokana na wengi hawana uhakika na kesho yao ya kisiasa.

Mwelekeo huo umeanza kukatisha tamaa kizazi cha sasa, huku baadhi yao kubadili mkondo wa kisiasa kuwa za mapambano badala ya mazungumzo.

Nchi kama Cameroon na Ethiopia, ambazo zimefanya chaguzi hivi karibuni, zimeripotiwa kuchukua hatua kali dhidi ya wapinzani, ikiwamo kuzuia mikutano na kuwakamata wanaharakati.

Hali kama hiyo imeshuhudiwa pia Zimbabwe, ambako vyama vya upinzani vimekabiliwa na shinikizo kubwa, ikiwamo kukamatwa kwa viongozi na wanaharakati, huku vikilalamikia mazingira yasiyo sawa wakati wa uchaguzi.

Katika baadhi ya matukio ya kusikitisha, mapambano ya kisiasa yamegharimu maisha ya wanasiasa na wanaharakati wa upinzani. Bara la Afrika limewahi kushuhudia vifo vya viongozi wa upinzani katika mazingira tata, huku uchunguzi ukiibua maswali mengi kuliko majibu.

Hali hiyo imejenga hofu miongoni mwa wanasiasa chipukizi na kudhoofisha ujasiri wa wananchi kuviunga mkono vyama hivyo hadharani.

Waliokumbwa na misukosuko ni pamoja na Miongoni mwa viongozi wa Afrika waliokumbwa na mashtaka ya uhaini katika siku za karibuni ni Rais wa zamani wa Sierra Leone, Ernest Koroma, aliyeshtakiwa Januari mwaka jana kwa tuhuma za kuhusika na jaribio la kumpindua Rais wa nchi hiyo. Viongozi wengine ni Ousmane Sonko wa Senegal, aliyeshtakiwa kwa kosa la uhaini kwa madai ya kuchochea machafuko; Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema, aliwahi kushtakiwa kwa uhaini baada ya kudaiwa kugoma kupisha msafara wa Rais wa wakati huo, Edgar Lungu (marehemu).

Nchini Uganda, mbunge na mwanamuziki maarufu, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, alishtakiwa Agosti, 2018 kwa uhaini pamoja na watu wengine 33, wengi wao wakiwa wanasiasa, baada ya msafara wa Rais Yoweri Museveni kushambuliwa kwa mawe. Kiongozi mwingine wa upinzani nchini humo, Kizza Besigye, ameendelea kuwa miongoni mwa wanasiasa waliokumbwa mara kwa mara na mashtaka ya uhaini, akishtakiwa miaka ya 2006, 2016 na 2024.

Mwanazuoni na mwanadiplomasia, Benson Bana akilizungumzia hilo alipofanya mahojiano na Mwananchi kwa simu, alisema jukumu la msingi la chama chochote cha siasa iwe cha upinzani au tawala, ni kujiandaa kushiriki uchaguzi na kuchukua madaraka kupitia sanduku la kura endapo Katiba na mifumo ya nchi imesimama vizuri.

Bana anasema vyama vya siasa vinapaswa kufanya kazi kama vitalu vya kuandaa viongozi kielimu, kimtazamo na kiitikadi, akisisitiza kuwa chama makini lazima kiwe tayari wakati wowote kupokea ridhaa ya wananchi kuongoza nchi.

“Kazi kubwa ya vyama ni kuandaa viongozi, kwa sababu wakati wowote chama kinaweza kuaminiwa na wananchi kuongoza dola,” anasema Bana.

Ingawa anasema katika baadhi ya nchi za Afrika, muundo wa kuanzisha na kuendesha vyama vya siasa haujakaa sawa, akitaja changamoto ya sheria za vyama vya siasa ambazo wakati mwingine humfanya Msajili wa Vyama kuwa kama mlezi wa vyama.

Kwa mujibu wake, nchi kama Nigeria huruhusu kuundwa kwa chama cha siasa wakati wowote na hata kuunda miungano, hali ambayo pia inaonekana Kenya, Ghana, Zimbabwe na Zambia.

Bana amesema udhibiti mkubwa wa kisheria kwa vyama vya siasa ni changamoto inayosababisha vyama vinavyochipukia kushindwa kujiandaa vya kutosha kuunda serikali, hali inayojitokeza pia Tanzania.

“Kwa mfano Tanzania, vyama vya upinzani bado havijawa tayari kushika dola. Hakuna chama kilichoandaa rasilimali watu wala itikadi madhubuti iliyofanyiwa upembuzi yakinifu na inayotekelezeka,” anasema.

Anaongeza kuwa vyama vya upinzani vimeendelea kuwa dhaifu licha ya kuwapo kwa miradi mbalimbali ya kuwaimarisha kupitia vyuo, akitolea mfano alipokuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulikuwa na mradi uliolenga kutoa elimu juu ya maana ya chama cha siasa, ilani na namna ya kujipanga kupata uungwaji mkono wa wananchi.

Bana anasema kinachosikitisha ni kuona vyama vingi vikiendelea kuwa mali ya watu binafsi, badala ya kuwa vyama vya wananchi na wanachama.

“Ndiyo maana vimekuwa vikionekana tu wakati wa uchaguzi. Ni vyama vya uchaguzi na wakati mwingine vya kiharakati zaidi kuliko kisera,” anasema.

Anaeleza kuwa hata katika nchi jirani kama Uganda, vyama vingi vinajengwa juu ya mtu mmoja badala ya taasisi imara yenye sera, ilani na itikadi.

“Chama kinapaswa kuwa na sera mbadala. Ukiwauliza wanapinga nini au wanapendekeza nini, hawana majibu,” anasema.

Mchambuzi wa siasa za Afrika, Hamduny Marcel anasema aina ya demokrasia ya vyama vingi inayoletwa kutoka mataifa ya Magharibi imekuwa changamoto katika baadhi ya nchi za Afrika kwa sababu wakati mwingine haiendani na tamaduni, mazingira na mila za wananchi.

Anasema pia, vyama vilivyoongoza harakati za uhuru vina hofu kwamba siasa za upinzani zinaweza kutumiwa na mataifa ya kibeberu kusababisha vurugu au kuyumbisha mamlaka ya nchi.

Hamduny anaongeza kuwa mazingira ya kisiasa hulazimisha baadhi ya vyama vya upinzani kutafuta msaada wa nje ili kupata madaraka, hali inayoweza kusababisha migogoro ya kisiasa na kukosa amani.

“Wakati mwingine, chama tawala kinapohisi kinatishiwa madaraka kutokana na makosa kama rushwa na ufisadi, hutumia nguvu za ziada kujilinda,” anasema.

Anasema bila vyama vya upinzani kuwa na ajenda mahususi, sera mbadala na muundo wa kidemokrasia unaoshirikisha wanachama kuanzia ngazi ya chini, ni vigumu kwao kupata ridhaa ya wananchi na kuongoza nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *