Dar es Salaam. Manukato ni kitu muhimu sana kwa mtu yeyote anayependa kuonekana nadhifu na mtanashati.

Pamoja na kusaidia kuboresha muonekano wa mtu kwa kumfanya anukie vizuri pia hutengeneza utambulisho wake anapokuwa katika eneo fulani.

Mbali na kuongeza mvuto, harufu nzuri hujenga kujiamini na kuacha taswira chanya kwa watu unaokutana nao.

Hata hivyo, si kila manukato yanafaa kwa kila mtu au kila mazingira, kabla ya kuyatumia ni muhimu kuzingatia mambo kadhaa ili kuepuka kuharibu umaridadi wako na hata kupata madhara ya kiafya.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na usafi wa mwili na nguo zako, hali ya afya ya ngozi yako, aina, hali ya hewa, mazingira, aina ya shughuli na ubora wa manukato.

Akizungumza na Mwananchi mfanyabiashara, mtaalam na mshauri wa bidhaa za manukato, Ally Bukuku anasema ili manukato yaweze kunukia vizuri na harufu hiyo kudumu kwa muda mrefu kabla ya kutumia ni vyema kuzingatia usafi wa mwili na nguo ulizovaa.

Bukuku anasema ili manukato yako yafanye kazi vizuri ni muhimu kuzingatia usafi wa mwili kwa kuhakikisha unaoga angalau mara mbili kwa siku bila kusahau usafi wa kinywa.

“Wakati wa kuoga hakikisha unatumia bidhaa sahihi na safisha vizuri mwili wako haswa katika maeneo ya makwapa na sehemu zenye mikunjo.

“Hakikisha mwili msafi kabla ya kuvaa manukato yako ili harufu ambayo sio rafiki isije kusafiri na marashi yako na ikafanya wanaokuzunguka wapate harufu mbaya”anasema.

Anasisitiza kuwa pamoja na usafi wa mwili ni muhimu kuhakikisha unapaka mafuta katika ngozi pia nguo unazovaa ni safi na nadhifu.

Anaeleza kuwa mtu anapopulizia marashi huku nguo zake zikiwa zinatoa harufu mbaya huweza kuchanganyika na harufu ya manukato na kuathiri utendaji kazi wake.

“Kuna baadhi ya watu wana tabia ya kurudia nguo bila ya kufua hili nalo ni la kuepuka kama unapenda kunukia vizuri wakati wote”anasema.

Anasema baada ya kuhakikisha usafi wa mwili na nguo ulizovaa. Ni muhimu pia kuzingatia hali ya hewa ya eneo ulilopo.

Bukuku anasema manukato yamegawanyika katika makundi makubwa mawili yani yale yenye harufu nzito mepesi ambayo husababishwa na aina ya malighafi zilizotumika kuitengeneza.

Anasema inashauriwa mtu anapokuwa kwenye mazingira ya joto kali atumie manukato yenye harufu nyepesi ya kawaida ambayo haitakera watu.

“Kutozingatia hali ya hewa ya mazingira ambayo mtu yupo au anaelekea kunaweza kufanya mtu akapulizia manukato ya gharama na bado asinukie vizuri au kuwa kero kwa wengine”anasema.

Pia anasema kabla ya kutumia aina fulani ya manukato ni muhimu kujiuliza wapi unakwenda, kufanya nini na muda gani ili iweze kuwa na chaguo sahihi la manukato.

Anatolea mfano mtu anayekwenda ofisini, shuleni au hospitalini ni vyema kutumia manukato yasiyo na harufu kali ili kuepuka kuwaudhi wengine.

 “Siyo vyema kwenda katika sehemu za kufanyia mazoezi ukiwa umejipulizia manukato yenye harufu nzito au kwenda katika sherehe nyakati za usiku ukiwa umepulizia manukato yenye harufu ya kawaida utafunikwa,”anasisitiza.

Vilevile anasisitiza mtu anapotaka kunukia vizuri kwa muda mrefu ni vyema kununua manukato yenye ubora kutoka sehemu zinazoaminika.

“Manukato yasiyo na ubora ni hatari kwa afya ya mtumiaji kwani huweza kusababisha changamoto katika ngozi pia harufu yake haidumu kwa muda mrefu”, amesema.

Nae mfanyabiashara wa manukato katika eneo la Mabibo mwisho jijini Dar es Salaam, Jenipher Mushi anasema inashauriwa kupulizia manukato kwa kiasi ili isiwe kero kwa wengine.

“Epuka kutumia manukato mengi kupita kiasi, matone machache tu yanatosha kutoa harufu nzuri na ya kuvutia cha muhimu ili kupata matokeo mazuri ni vema kutumia ile yenye ubora zaidi,”amesema.

Pia anasema wakati wa kutumia manukato ni muhimu kuzingatia maeneo ya shingoni, nyuma ya masikio au kwenye vifundo vya mikono.

Vilevile anasisitiza kuzingatia uhifadhi wake kwa kuhakikisha unaihifadhi sehemu yenye baridi na pasipo na mwanga mkali ili yadumu kwa muda mrefu.

Kwa nini ni muhimu kutumia manukato

Kwa mujibu wa Bukuku anasema mtu anapotumia manukato humsaidia mtumiaji kuboresha muonekano wake anapokuwa mbele ya watu.

Pia inamuongezea thamani kwani baadhi ya watu humhusianisha mtu kutokana na namna anavyonukia.

“Baadhi ya watu unaweza kuwa nae karibu kutokana na namna anavyonukia wakiamini kuwa yeye ni wa hadhi ya juu”amesema.

Vilevile inamsaidia kumtambulisha kutokana na namna anavyonukia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *