Dar es Saalam. Airtel Afrika imeweka historia mpya katika sekta ya mawasiliano barani Afrika baada ya kuwa kampuni ya kwanza kuanzisha huduma ya setilaiti moja kwa moja kwenye simu janja kupitia teknolojia ya Starlink Direct to Cell, kwa ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya SpaceX.

Hatua hiyo itahusisha nchi 14 ambako Airtel Africa inatoa huduma, zikiwa na zaidi ya wateja milioni 174, na inalenga kuvunja kabisa vikwazo vya mawasiliano kwa kuwafikia wananchi wanaoishi katika maeneo ya mbali na magumu kufikika ambayo kwa muda mrefu yamekuwa nje ya mtandao wa kawaida wa mawasiliano ya ardhini.

Kwa mara ya kwanza barani Afrika, wateja wa mtandao wa simu wataweza kuunganishwa moja kwa moja na setilaiti bila kutegemea minara ya simu, mradi tu wawe na simu janja zinazokidhi mahitaji ya kiteknolojia. Huduma hiyo itatumia setilaiti za Starlink, mtandao mkubwa zaidi wa mawasiliano ya 4G duniani kwa upana wake.

Kwa mujibu wa Airtel Africa, utoaji wa huduma hiyo unatarajiwa kuanza mwaka 2026, ukihusisha awamu ya mwanzo ya ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) na matumizi mahsusi ya data.

Aidha, kupitia Starlink Direct to Cell, simu za mkononi zitapata intaneti ya kasi ya juu inayokadiriwa kuwa mara 20 zaidi ya viwango vya sasa, hatua inayotarajiwa kuleta mapinduzi katika upatikanaji wa huduma za kidijitali, hususan vijijini.

Utekelezaji wa mpango huo utafanyika kwa kuzingatia taratibu na vibali vya mamlaka za udhibiti katika kila nchi husika. Zaidi ya setilaiti 650 za Starlink zinatarajiwa kutumika kuhakikisha mawasiliano ya uhakika kwa wateja walioko maeneo yasiyofikiwa na miundombinu ya kawaida.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo ya kihistoria, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar, ameema kampuni hiyo inaendelea kuonesha uongozi wake katika uvumbuzi wa teknolojia barani Afrika.

“Kwa kuwa kampuni ya kwanza Afrika kuanzisha huduma ya Starlink Direct to Cell, tunaimarisha dhamira yetu ya kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika mawasiliano. Teknolojia hii inaongeza nguvu kwenye mtandao wetu wa ardhini kwa kufikia hata maeneo ambayo ni magumu kuyahudumia kwa njia za kawaida,” amesema.

Naye Makamu wa Rais wa Mauzo wa Starlink, Stephanie Bednarek, amesema ushirikiano huo unafungua ukurasa mpya wa mawasiliano barani Afrika.

“Kwa mara ya kwanza, mamilioni ya Waafrika wataweza kuwasiliana moja kwa moja kupitia setilaiti hata wakiwa mbali na miundombinu ya ardhini. Tunajivunia kushirikiana na Airtel Africa katika kuleta teknolojia hii ya mapinduzi,” amesema.

Hatua hiyo inaiweka Airtel Africa kama kinara wa uvumbuzi wa mawasiliano barani Afrika, huku ikichangia kwa kiasi kikubwa kupunguza pengo la kidijitali na kuwezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma muhimu za mawasiliano na intaneti bila kujali wanakoishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *