Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria sawa na tarehe 18 Disemba 2025.
Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa muitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria.
Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania.
Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake.

Katika siku kama ya leo miaka 87 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia.
Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia.

Tarehe 18 Disemba miaka 46 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake.
Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu.
Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu unasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho.

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita Dakta Muhammad Mufatteh alimu, mwanaharakati na mwanamapambano wa Kiirani aliuawa shahidi na makundi ya kigaidi.
Baada ya kumaliza masomo yake ya kimsingi alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum. Sambamba na kusoma masomo ya dini, Muhammad Mufatteh alikuwa akisoma pia katika Chuo Kikuu cha Tehran na kufanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika falsafa yaani PHD.
Baada ya kupata shahada hiyo akaanza kufundisha kama mhadhiri huku akiendesha harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini Iran.

Leo Disemba 18 dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya Wahamiaji!
Kutokana na kuongezeka idadi ya wahamiaji duniani kote, mwaka 1990 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Haki za Wafanyakazi Wote Wahamiaji na Wanachama wa Familia Zao. Takriban muongo mmoja baadaye, mwaka wa 2000, Disemba 18 ilitangazwa kuwa siku ya kuadhimisha mchango wa wahamiaji na msaada wa uhamiaji katika maendeleo.
Siku hii inatuhimiza kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha kwamba uhamiaji ni uzoefu salama na chanya kwa pande zote.
Wahamiaji wanatoa mchango mkubwa duniani katika maendeleo ya kiuchumi na kiutamaduni, na wanatumiwa kwenye majeshi ya ulinzi, matibabu, kufanya kazi ngumu, na pia ni mabalozi wanaokuja na fikra na mawazo mapya.
