Kongamano lililofanyika Kampala, Uganda limewaleta pamoja wanasiasa, wasomi na wanadiplomasia kutoka mataifa ya ndani na nje ya Afrika.

Azma yao ni kuweka shinikizo kwa mashirika ya Afrika na pia kimataifa kuchukua hatua na kufanya maamuzi ya makusudi kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, badala ya kulizungumzia tu suala hilo. Akizungumza katika kongamano hilo, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli ameelezea umuhimu wa wadau wa Afrika kuanzisha shinikizo hilo.

”Hata ukienda Sudan kwa sasa utakuta watu wanavyouawa, na sio kwamba ni vita vya kikabila, bali ni mali ambayo mtu anayeitaka hasa kutoka mataifa ya kigeni. Hiki ni kitu tunatakiwa kukitambua sisi kama Waafrika.”

Chini ya kaulimbiu ya “Sudan kwenye uwanja wa mapambano, kupinga ubepari” washiriki waliukosoa hasa Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE kwa kusaidia kuendeleza vita hivyo kwa madai ya kuwapatia silaha wanamgambo wa RSF, pamoja na misaada mingine.

Wamedai kuwa Marekani ambaye ni mshirika wa nchi hiyo nayo haijajishughulisha ipasavyo katika juhudi za kukomesha vita hivyo.

AU na UN zatakiwa kuogoza juhudi za kukomesha vita Sudan

Washiriki hao wamevitaja vita vya Sudan kuwa vita dhidi ya Afrika, kwani wale wanaojitakia makuu wakifaulu kuporomosha utawala na uthabiti wa nchi hiyo, watalenga nchi jirani za Kaskazini, Kati na Mashariki mwa Afrika.

Sudan Joda 2014 | Mapigano makali yasababisha maelfu kukosa makaazi Sudan
Raia wa Sudan waliokosa makaazi kufuatia vita kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF Picha: Ashraf Shazly/AFP

Kongamano hilo lilikamilika kwa kutoa tamko la Azimio la Kampala linaloutaka Umoja wa Afrika pamoja na Umoja Mataifa kuongoza katika juhudi za kukomesha maafa Sudan na kurejesha utawala wa kiraia, kama anavyofafanua kwa undani Mwenyekiti wa kongamano hilo, Mugabe Rubahamya.

”Kuendelezwa kwa vita hivi kunawezeshwa na misaada ya moja kwa moja na mingine kutoka UAE ambalo linataka kuidhibiti Ghuba ya Uajemi kijeshi na kiuchumi.”

Balozi wa Sudan nchini Uganda, Ahmed Ibrahim Ahmed pia amezungumza katika kongamano hilo.

”Wakati umefika kwa watu wa Afrika tujitokeze kupigana dhidi ya wale wanaoingilia masuala yetu, iwe Sudan au kwengineko.”

Tangu kuzuka kwa vita vya Sudan mwaka 2023, watu zaidi ya milioni moja wameyakimbia makaazi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *