
Dar es Salaam. Kutokana na ongezeko la mahitaji usafiri katika eneo la kanda ya ziwa Shirika la ndege la ndege la Auric Air Services imeanzisha safari nne za ndege kwa wiki kati ya Dar es Salaam, Mwanza na Kahama.
Safari hizo zitakuwa ni kila Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili, Ndege itakayokuwa inatumika ni Bombardier Dash 8-300 yenye uwezo wa kubeba abiria 50.
Ndege itakuwa ikielekea Mwanza kupitia Kahama, muda wa safari kati ya Dar na Kahama utakuwa takribani masaa mawili, Kahama kwenda Mwanza dakika 30 na Mwanza kwenda Dar itakuwa masaa mawili na dakika 10.
Akizungumza kuhusu kuanza kwa safari hizo Mkurugenzi wa mauzo wa shirika hilo Deepesh Gupta alisema tofauti yao na mashirika mengine yanayotoa usafiri katika ruti hiyo ni muda wa safari kwani wao wanasafiri nyakati za mchana na jioni ambako kulikuwa hakuna safari.
Gupta alisema ruti hizo mpya zinawapa nafasi ya kuongeza mchango wao katika sekta ya anga wakiwa na ndege 25 zikiwemo kubwa nne na za anasa (luxury) 2.
Kuhusu ushindani wa soko katika sekta hiyo alisema ukubwa ulilonalo shirika la ndege la Tanzanzania (ATCL) hauleti ugumu wa wao kushindani isipokuwa linawasaidia na wao kupata wateja zaidi.
“Sio kwamba utawala wa soko wa ATCL ni maumivu kwetu sisi wadogo isipokuwa kadri linavyokuwa na safari nyingi za nje linaleta abiria ambao na sisi tunawapeleka katika maeneo ambayo wao hawafiki hususani kwa safari za kitalii,” alisema Gupta.
Kwa upande wake Afisa mipango wa Shirika hilo Asha Mzuri alisema ongezeko la uhitaji wa usafiri wa anga kwa sehemu kubwa limetokana na maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali katika viwanja vya ndege.
“Soko la abiria wa anga linakuwa, miundombinu inaboreshwa na hata ufanisi wa mashirika nao unaongezeka, shukrani kwa Serikali kwa kuunga mkono ukuaji wa sekta hii,” alisema Mzuri.