BAADA ya kukosekana nusu msimu kiungo mkabaji wa KMC, Baraka Majogoro anatarajia kuanza kuitumikia timu hiyo mapema mwezi ujao baada ya ITC yake kupatikana ikitokea klabu ya Chippa United ya Afrika Kusini.

Usajili wa kiungo huyo ulishindwa kukamilika wakati wa dirisha kubwa la usajili kutokana na kuchelewa kufika kwa ITC yake ikitokea Afrika Kusini ambako hakumaliza mkataba baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya KMC kimelithibitishia Mwanaspoti kuwa Majogoro sasa atakuwa sehemu ya kikosi kinachotakiwa kuipambania KMC baada ya kukamilisha usajili wake ambao ulikwama tangu mwanzo wa msimu licha ya kumnasa akiwa mchezaji huru.

“Ni kweli Majogoro hakuwa sehemu ya kikosi chetu kutokana na ITC yake kuchelewa, tulishindwa kumsajili kwenye mfumo sasa hili limekamilika baada ya juhudi kubwa ya uongozi na mchezaji mwenyewe ambaye alikuwa anatamani nafasi ya kuendelea kucheza,” kilisema chanzo hicho;

“Mchezaji yupo fiti kwani alikuwa akiendelea na mazoezi sambamba na timu kilichokuwa kinakosekana ni mechi za mashindano hivyo tunatarajia ubora tuliokuwa tunaukosa utapatikana kutoka kwake eneo la kiungo.”

Majogoro aliwahi kutamba na klabu kadhaa hapa nchini ikiwamo Mtibwa Sugar na Biashara United na kisha akatimkia huko Afrika Kusini.

Kiungo huyo alikuwa na wakati Bora kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini na kujipatia uzoefu wa kutosha.

Kwa Sasa amerejea nyumbani Tanzania huku ikiwa bado hajaonyesha makeke yake kutokana na kuchelewa kuingia kwenye mfumo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *