Benki ya Ushirika (Coop Bank) imezindua rasmi CooPesa, suluhisho la kwanza la benki la kidijitali kupitia simu ya mkononi, hatua inayoweka alama muhimu katika safari ya benki hiyo kuelekea mageuzi ya kidijitali na utoaji wa huduma zinazomlenga mwanachama wa ushirika.

Uzinduzi wa CooPesa unalenga kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali miongoni mwa  wanachama, kuboresha ufanisi wa kiutendaji, na kuchangia kwa kiasi kikubwa ajenda ya kitaifa ya ujumuishaji wa kifedha na ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo akizungumza na wageni waalikwa katika hafla ya uzinduzi wa suluhisho la kidijitali la CooPesa jijini Dodoma juzi.

Kuanzishwa kwa CooPesa kunaonyesha dhamira ya Coop Bank katika kutoa huduma za benki salama na rahisi. Suluhisho hili litawawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za benki wakati wowote na mahali popote kupitia simu zao za mkononi.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah, amesema kuwa CooPesa ni suluhisho la kidijitali litakalobadilisha namna ya utoaji wa huduma za benki kwa kurahisisha miamala ya kila siku huku likiimarisha ujumuishaji wa kifedha kote nchini.

Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah akizungumza na wageni waalikwa katika hafla ya uzinduzi wa suluhisho la kidijital la CooPesa jijini Dodoma juzi.

“Suluhisho hili litaaongeza ujumuishaji wa kifedha katika ngazi ya chini kote nchini na linaunga mkono kikamilifu Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050. Dhamira yetu ni kuzifikia familia milioni 10,” amesema na kuongeza:

“CooPesa ni zaidi ya programu ya benki kwa simu. Ni jukwaa la kimkakati linaloleta huduma za benki karibu zaidi na wanachama wetu. Kupitia suluhisho hili, tumejizatiti kuongeza urahisi, upatikanaji, na ufanisi katika benki ya ushirika.”

Ng’urah amesema CooPesa itamwezesha mtumiaji kuangalia salio, kulipa bili, kununua muda wa maongezi, pamoja na kufanya malipo ya Serikali. Amesisitiza kuwa jukwaa hilo limejengwa kwa mifumo imaraya kiusalama ili kuhakikisha usalama na faragha ya taarifa za kifedha za wateja.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Daniel Chongolo, Waziri wa Kilimo, ameipongeza Coop Bank kwa kufanikisha hatua hiyo muhimu ya kidijitali na kusisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuunga mkono ukuaji wa benki hiyo.

Ameipongeza pia benki hiyo kwa mafanikio yaliyopatikana ndani ya mwaka mmoja tangu kuanzishwakwake na kuhimiza menejimenti ya benki hiyo kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa za ulinzi ili kuhakikisha usalama wa fedha za wanaushirika na wateja wake, sambamba na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika sekta ya fedha.

Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah akizungumza na wageni waalikwa katika hafla ya uzinduzi wa suluhisho la kidijital la CooPesa jijini Dodoma juzi.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Coop Bank, Dk Joseph  Witts, aliipongeza menejimenti ya benki kwa utekelezaji makini wa mkakati wa benki uliowezesha Coop Bank kuwa miongoni mwa benki zinazokua kwa kasi zaidi nchini.

“Takwimu za hivi karibuni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa Coop Bank ni miongoni mwa benki zinazokua kwa kasi zaidi nchini Tanzania. Wakati benki nyingine zinatembea, Coop Bank inapaswa kukimbia,” ameongeza.

Dk Witts aliitaka menejimenti ya Coop Bank kuendelea kubuni bidhaa mahsusi zitakazosaidia kuziba pengo la ujumuishaji wa kifedha.Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wengine waandamizi wa Serikali, wabunge, viongozi wa vyama vya ushirika, wadau wa sekta binafsi, pamoja na washirika mbalimbali, jambo lililoonyesha umuhimu wa ubunifu wa  kidijitali katika kuimarisha sekta ya ushirika na fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *