Diwani wa Kata ya Chanika Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga , Dkt. Habibu Mbota amefanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule Shikizi iliyopo Chanika, mtaa wa Azimio, ambapo amebaini changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa mradi huo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mbota amebaini kuwa baadhi ya wazabuni hawazingatii ubora wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi, hali inayohatarisha viwango vinavyotakiwa.

Aidha, Mbota amesema kuwa muda wa kukamilika kwa mradi hauzingatiwi ipasavyo, huku baadhi ya majengo yakiwa bado katika hatua ya msingi na mengine yakiwa yamesimama kabisa.

Mbota amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 48 pekee, licha ya kuwepo kwa kikomo cha kukamilika ifikapo tarehe 30 Desemba 2025, hali hiyo imeibua wasiwasi mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa fedha zote kwa ajili ya mradi huo kiasi cha shilingi milioni 3,307,000/=.

Kutokana na hali hiyo, Dkt. Mbota amewaagiza wahusika wote wanaosimamia utekelezaji wa mradi huo kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati, kwa kuzingatia ubora unaotakiwa.
#StarTvUpdate

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *