HUKO mtaani mashabiki na wapenzi wa Simba, wamekaa mkao wa kula kusikilizia ataletwa kocha gani wa kuinoa timu hiyo kwa ngwe zilizosalia za Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya ndani, lakini taarifa mpya ni mabosi wa klabu hiyo kwa sasa wamegawanyika kuhusu kocha Miguel Gamondi.

Hesabu kubwa za Simba zipo kwa kocha huyo wa zamani wa Yanga anayeinoa kwa sasa Singida Black Stars, lakini akiwa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 itakayoanza rasmi Jumapili hii na kukamilika Januari 18, mwakani.

Kama Mwanaspoti lilivyowajulisha mapema, Gamondi ameomba kazi ya kuifundisha timu hiyo kwa mara ya pili, lakini kumeibuka mvutano uliozalishwa na tofauti wa kimtazamo juu ya kocha huyo wa zamani wa watani wao Yanga.

Taarifa kutoka Simba ni kwamba Gamondi amewagawa mabosi wa klabu hiyo katika makundi mawili makubwa na kundi la kwanza linaona kocha huyo ni mwafaka kwao, wakiangalia rekodi alizokuwa nazo tangu akiwa Yanga akiwapa ubingwa tofauti.

Mbali na hoja hiyo ya kundi hilo pia vigogo hao wanaona timu yao inahitaji kocha mwenye uzoefu kama Muargentina huyo, endapo tu atapewa kila kitu anachohitaji katika kikosi hicho na kuirejesha timu katika mstari kama ilivyokuwa miaka kadhaa nyuma, ikiwamo kurejesha mataji.

“Wanaoona kocha huyu anatufaa wametoa mtazamo huo, Gamondi atatufaa kwa kuwa amefanya makubwa mazuri pale upande wa pili na hata Singida ndani ya muda mfupi amewapa Kombe la Kagame na kuipeleka timu hiyo makundi ya michuano ya CAF,” amesema mmoja wa mabosi wa klabu hiyo aliyeongeza;

“Wanaona pia kwa kikosi chetu kwa sasa kinahitaji kocha mzoefu, mkali atakayewanyoosha wachezaji wetu, tofauti na hawa makocha wachanga ambao wamepita hivi karibuni, bado hoja hizo zinashindana na wengine.”

Pia bosi huyo alifichua kwamba wanaopinga Gamondi kutopewa nafasi wanadai kocha huyo ambaye aliwapiga mabao 5-1 akiwa Yanga, bado ana kumbukumbu nzuri na timu hiyo ya zamani lakini anatokea pia timu rafiki na watani wao hao.

Mbali na hoja hiyo inaelezwa, misimamo ya kocha huyo haitaweza kupita kirahisi kwa baadhi vigogo wenzao hatua ambayo anaweza kuwa kocha mwingine atakayeingia katika migogoro kirahisi kama ilivyokuwa kwa Dimitar Pantev.

“Kundi lingine ni lile linaloona tutafute kocha mwingine bora mbali na Gamondi, wanasema yaani kocha atufunge tano halafu tumchukue tena akiwa anatoka Yanga akahamia Singida na tulipomtaka mara ya kwanza akazuiwa kisiasa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kuna hoja ya misimamo ya Gamondi, tukubaliane shida yetu nyingine ni mgawanyiko wa viongozi uliopo, lakini Gamondi ana hulka ya anachokitaka lazima kiwe je kwa baadhi yetu huku ndani watakubaliana naye au ataondoka kwa muda mfupi.”

“Hoja yao nyingine ni kwamba sisi tunataka kocha haraka, aje aanze kupambana na wachezaji wetu huyo Gamondi yupo Morocco kwa sasa hata tukisema atawahi tutamtarajia kuanzia mwakani, kumbuka muda hautakuwa rafiki sana kwa kuwa Januari hiyo hiyo tunatakiwa kuwafuata Esperance.”

Hata hivyo, taarifa nyingine zilisema kocha huyo tayari ameanza kuaga mapema Singida kutokana na kuwaambia mabosi wake, TFF ina malengo ya muda mrefu naye, iwapo ataiwezesha Stars kufanya maajabu AFCON 2025 ikipangwa kundi moja na Nigeria, Uganda na Tunisia.

“Jamaa ameanza kuaga, lakini akisema ni kutokana na kuzungumza na TFF na kumtaka aiwezeshe Stars ifanye makubwa Morocco, kwani ina malengo naye ya muda mrefu, ingawa taarifa aliomba kazi Simba inaweza kuwa sababu, kwani inadaiwa mabosi wa klabu hiyo wanamtaka zaidi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *