Mwisho wa juma lililopita, jeshi la Israel lilitoa onyo kwa raia wanaoishi kusini mwa Lebanon, likisema litashambulia miundombinu inayodaiwa kumilikiwa na Hezbollah katika mji wa Yanouh. Israel iliwataka wakazi wa eneo hilo kuhama mara moja kwa ajili ya usalama wao.

Hata hivyo, katika tukio lililoelezwa na vyombo vya habari vya Israel kuwa la nadra na lisilo la kawaida, jeshi la Lebanon liliomba kuruhusiwa kukagua majengo yaliyotajwa badala ya Israel kufanya mashambulizi ya angani. Israel ilikubali ombi hilo na kusitisha shambulio lililokuwa limepangwa.

Tarehe 31 Desemba mwaka huu ndiyo muda uliowekwa na Israel kwa mamlaka za Lebanon kuhakikisha kuwa Hezbollah imepokwa silaha na maghala yake yote ya silaha yameteketezwa. Jeshi la Lebanon linasema tayari limefanya oparesheni kadhaa za kulipua maghala ya silaha, ingawa waangalizi wa kimataifa wanasema ni vigumu kuthibitisha utekelezaji kamili wa hatua hizo.

Licha ya kuwepo kwa usitishaji mapigano uliopatanishwa na Marekani na Ufaransa mwezi Novemba, Israel imeendelea kushambulia maeneno nchini Lebanon karibu kila siku. Zaidi ya raia 120 wa Lebanon wameuawa tangu wakati huo, huku wanajeshi wa Israel wakiendelea kuwepo katika baadhi ya maeneo ya mpakani. Pia kuna mvutano kuhusu iwapo zoezi la kupokonya silaha linapaswa kufanyika kusini mwa Lebanon pekee au kote nchini.

Pande hasimu zinalaumiana kwa kukiuka masharti ya usitishaji vita

Israel na Lebanon zimekuwa zikilaumiana kwa kukiuka masharti ya usitishaji mapigano. Mchambuzi mkuu wa masuala ya Lebanon katika taasisi ya Crisis Group, David Wood, anasema hali hiyo imesababisha mkwamo hatari.

Libanon Beirut 2025 |
Marekani imekuwa mshirika wa karibu wa Israel katika kuiwekea shinikizo Lebanon, Picha: Anonymous/Middle East Images/IMAGO

“Israel inasema itaondoa wanajeshi wake Lebanon pale tu Hezbollah itakapopokonywa silaha. Hezbollah nayo inasema itafanya hivyo pale tu wanajeshi wa Israel watakapoondoka na mashambulizi kusitishwa, licha ya ukweli kwamba Israel ina nguvu kubwa ya kijeshi,” anasema Wood.

Marekani, ambayo imekuwa mshirika wa karibu wa Israel katika kuiwekea shinikizo Lebanon, imeonya kuwa itapunguza ufadhili wake kwa jeshi la Lebanon endapo halitaharakisha zoezi la kuipokonya silaha Hezbollah. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kudhoofisha zaidi uwezo wa jeshi hilo.

Mshauri mwandamizi wa Baraza la Atlantiki kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati, Nicholas Blanford, anasema mashambulizi yanayoendelea ya Israel yanahujumu juhudi za kuinyang’anya silaha Hezbollah.

Anasema kuwa iwapo Israel ingeondoa wanajeshi wake na kupunguza mashambulizi, shinikizo dhidi ya Hezbollah kuweka silaha chini lingeongezeka zaidi, badala ya hali ya sasa ambayo inaongeza mvutano na kuhatarisha uthabiti wa kisiasa wa Lebanon.

Kwa sasa, Lebanon inaonekana kunaswa kati ya masharti magumu ya kimataifa, shinikizo la kijeshi la Israel na hofu ya mgawanyiko wa ndani—hali inayotia doa mustakabali wa usitishaji huo wa mapigano. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *