Uvumbuzi wa huduma mbadala za kifedha unaendelea kuongezeka kila siku kwa mtindo mbalimbali ikiwamo kuongezeka idadi ya taasisi zinazotoa huduma hizo kwa njia ya kielektroniki, mitandao ya simu, huduma za kibenki na mengine.

Uvumbuzi huu mpya unachagiza urahisi na kuongeza idadi ya watumiaji rasmi wa huduma za kifedha na kukuza ujumuishi.

Moja kati ya uvumbuzi huo ni kuanza kwa utoaji wa huduma za bima kwa mfumo wa Kiislam maarufu kama Takaful, ambapo hivi karibuni baadhi ya makampuni yameanza kutoa huduma za bima kwa mtindo huo.

Takaful ni mfumo wa kutoa huduma mbalimbali za bima kama ilivyo mtindo wa kawaida ambapo mteja anaweza kupata huduma mfano bima ya vyombo vya moto, bima ya ajali, bima ya moto, bima ya maisha na nyinginezo. Muhitaji wa bima atachagua sera na mkataba anaotaka (insurance policy) ambayo itaelekeza ni kiasi gani cha kulipia (premium) kulingana na aina ya bima anayokata.

Upande wa kwanza, mtindo wa Takaful na bima za kawaida zote mbili msingi wa uchangiaji wake wa fedha unafanana, unatokana na mfumo wa michango kutoka kwa wateja waliochangia bima (pooling of risks), mchangiaji yeyote anapofikwa na janga iliyokatiwa bima, baada madai yake kuthibitishwa, kampuni ya bima inatumia kiasi hicho kufidia hasara iliyopatikana kwa muhusika.

Hata hivyo, tofauti ya msingi kati ya Takaful na bima ya kawaida ipo katika falsafa ya uendeshaji, muundo wa mikataba, na namna ya kusimamia hatari, faida, na uwekezaji. Na ndio hapo uendeshaji wake ni muhimu kuzingatia kanuni za kifedha kulingana na mafundisho ya Uislam.

Mwanazuoni mashuhuri wa sayansi ya uchumi na fedha wa kisilaam Taqi Usman (1998), anaeleza  biashara ya bima ya Takaful ina misingi mikuu minne ambayo ni kuepuka riba, mazingira yasiyotabirika, kuleta usawa baina ya kampuni ya bima na wachangiaji wa bima, na uwekezaji unaokubalika kuwa ni halali.

Kutokana na misingi hiyo, kwanza, mteja anayekata bima katika mtindo wa Takaful anahitajika kuingia makubaliano baina yake na kampuni ya bima ambayo yatajulikana kwa lugha ya kimkataba kama “Tabarru”.

Ki-sharia makubaliano hayo yanamaanisha kuwa mchangiaji anayekata bima anakubali kwa hiari michango yake (premiums) itatumika kufidia hasara iliyokatiwa bima ikitokea kwake au kwa wateja wengine.

Pili, kuondoa mazingira ya biashara ya bima ambayo yanatafsiriwa kuwa yasiyotabirika. Kwa mfano, ajali iliyokatiwa bima isipotokea mchangiaji atakua amepoteza michango yake.

Kimantiki ni sawa na ilivyo michezo ya upoteaji wa matokeo ya mpira wa miguu (betting), “mkeka ukichanika” hupati kitu. Jambo hili kanuni za fedha za kislam zinalikataza kama jambo lisilofaa kwa kitaalam huitwa gharar.

Kwa msingi huo imewekwa katika msingi kwamba mteja asipoteze kabisa. Kampuni inayoendesha bima ya Takaful itahitajika kuwa na mfuko wa uwekezaji (Takaful Investment Fund), ambapo michango iliyopokelewa kutoka kwa wanachama au wateja waliokata bima itawekezwa katika biashara mbalimbali zinazokubalika kuwa ni shughuli halali kwa mujibu wa Sharia.

Kulifanya hilo likubalike ki-Sharia, katika mtindo wa Takaful mchangiaji aliyekata bima atasaini mkataba wa pili unaojulikana kama “Mudaraba” baina yake na kampuni ya bima, mkataba huo unatengeneza ushirikiano wa kibiashara baina ya mchangiaji na kuiruhusu kampuni ya bima kutumia michango ya waliokata bima kuwekeza katika biashara mbalimbali.

Vilevile, kampuni ya bima inalipia gharama mbalimbali za uendeshaji, mchangiaji aliyekata bima atasaini mkataba wa tatu unaojulikana kama ‘Wakala’, ambao unaruhusu kampuni ya bima kuchukua tozo au kukata gharama mbalimbali ili kufidia uendeshaji kutoka katika michango au mfuko wa uwekezaji.

Mtindo wa bima wa Takaful umeanza kutumika katika mataifa mbalimbali duniani katika nchi za Ulaya, Asia, Mashariki ya Kati, na Mashariki ya Mbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *