Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, wameitembelea Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” iliyokita kambi jijini Cairo nchini Misri.

Waziri Kombo na Profesa Kabudi, wameitembelea kambi hiyo na kuikabidhi bendera ya Taifa, ikiwa ni ishara ya kuitakia kila la kheri na kuitia shime kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) huko nchini Morocco kinachotarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 21 kwa mwenyeji Morocco kuivaa The Comoros.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Kombo amewasihi wachezaji wa stars kutanguliza uzalendo kwanza na kuipigania bendera ya Taifa kwa jasho na damu ili kuiletea heshima Tanzania.

Kwa upande wake, Prof. Kabudi, amekiahidi kikosi hicho ushirikiano wa kila aina katika kuhakikisha kinafanya vyema katika michuano hiyo mikubwa na yenye heshima kubwa sio tu barani Afrika bali duniani kwa ujumla.

Aidha, Prof Kabudi amewahimiza Watanzania kuipenda na kuipa moyo timu yao ya Stars kwa kuwashangilia kwa wale watakaokuwa na nafasi kwenda kujiunga nao kwenye mechi zao zote watakazocheza huko nchini Morocco.

Ikumbukwe kwamba kikosi cha Taifa Stars kipo kundi C lenye timu za Nigeria, Tunisia na Uganda na kitaanza michuano hiyo kwa kucheza na moja ya timu bora barani Afrika timu ya Taifa ya Nigeria Desemba 23.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *