Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametangaza kwamba nchi yake haitarudi nyuma na wala  haitaachana na  misimamo yake kuhusu Gaza.

Kulingana na Pars Today, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema hayo katika mazungumzo na wanafunzi huko Istanbul na kusisitiza mwendelezo wa utendaji wa nchi hiyo wa kuunga mkono Gaza.

Erdogan alisisitiza: “Hakutakuwa na suala kurudi nyuma, na tukirudi nyuma, tutawajibika kwa Mungu na Gaza.” Akizungumzia hotuba yake aliyoitoa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Erdogan amesema: “Ujumbe wa Israel ulikuwa umekaa mezani mbele yangu, na nilitoa hotuba hiyo huku nikiwatazama moja kwa moja machoni. Hatuogopi chochote.”

Akizungumza na mabalozi wa Uturuki siku ya Jumanne, Erdogan alisema: “Kabla ya mauaji ya halaiki, idadi ya watu wa Gaza ilikuwa karibu milioni 2.3. Zaidi ya tani 200,000 za mabomu zilimiminwa kwenye mji huo mdogo. Ziliisawazisha kabisa Gaza kwa zaidi ya mara 14 ya mabomu yaliyorushwa Hiroshima.” Pia aliongeza: “Mbinu ya utulivu ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesaidia kwa kiasi kikubwa kudumisha usitishaji mapigano licha ya kuongezeka kwa ukiukwaji wa Israel.”

Erdogan amesema: “Katika kipindi kilichoko mbele yetu, tutaendelea na njia yetu ya kuwaunga mkono watu wa Palestina kwa azma thabiti.”

Msimamo wa Rais Erdogan wa Uturuki kutorejea nyuma katika misimamo yake kuhusu Gaza unaonekana kutegemea mchanganyiko wa utambulisho wa kihistoria, kanuni za kiitikadi, maslahi ya kijiografia, uhusiano na Hamas, mashinikizo ya ndani na ya umma wa Kiislamu, na sera huru ya kigeni. Msimamo huu pia ni sehemu ya sera za kigeni za Uturuki ili kuimarisha nafasi yake kama nguvu ya kikanda na mtetezi wa haki za Palestina.

Maandamano ya wananchi wa Uturuki ya kuunga mkono Palestina

Katika miaka ya hivi karibuni, Uturuki imekuwa ikiionyesha Gaza kama sehemu ya utambulisho wake wa kisiasa na kidini katika sera yake ya kigeni. Serikali ya Erdogan imesisitiza mara kwa mara kwamba, suala la Palestina, na hasa Gaza, si kadhia ya kibinadamu tu, bali pia ni wajibu na jukumu la kihistoria kwa Uturuki. Mtazamo huu umejikita katika mila ya Othmaniya na uhusiano wa kihistoria na ardhi za Kiarabu. Erdogan na chama chake cha Uadilifu na Ustawi, wakitegemea urithi huu, wanajitambulisha kuwa watetezi wa Waislamu waliokandamizwa, na Gaza ni ishara ya mbinu na utendaji huu.

Kwa mtazamo wa kijiografia, Uturuki inajaribu kuimarisha msimamo wake katika milingano ya Asia Magharibi. Uwepo hai katika suala la Gaza huruhusu Ankara kutambuliwa kama mchezaji muhimu katika mchakato wa amani au usimamizi wa migogoro, pamoja na mataifa yenye nguvu kama vile Qatar na Misri. Utendaji huu ni muhimu kwa Uturuki kwa sababu kwa njia hiyo inaweza kuongeza ushawishi wake katika ulimwengu wa Kiarabu na kupata nafasi maalum dhidi ya wapinzani kama vile Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Fauka ya hayo, kwa kuunga mkono Palestina, Uturuki inaweza kuimarisha uhusiano wake na nchi za Kiislamu na hata maoni ya umma ya ulimwengu wa Tatu.

Jambo jingine ni uhusiano wa karibu wa Uturuki na harakati ya Hamas. Ingawa nchi za Magharibi zinaiona Hamas kama kundi la kigaidi, lakini Uturuki inaitambulisha kama harakati halali ya muqawama inayopigania ukombozi na matakwa halali. Mbinu hii imeipa Ankara jukumu maalum katika mazungumzo na upatanishi, kwani inaweza kuanzisha mawasiliano na makundi ambayo wengine hawawezi kujadiliana nayo. Kujiondoa kutoka katika nafasi hii kuna maana ya kupoteza sifa hii ya kidiplomasia.

Gaza inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

Maoni ya umma ndani ya Uturuki pia yana mchango muhimu. Jamii ya Uturuki kwa ujumla iko hasasi na ina unyeti maalumu na suala la Palestina, na himaya na uungaji mkono kwa Gaza kunamfanya kuwa mahabubu miongoni mwa makundi mbalimbali ya watu yule anayelipigania hilo. Kwa kudumisha msimamo huu, Erdogan anaweza kuimarisha msingi wake wa kijamii na kujionyesha kama kiongozi anayewatetea Waislamu. Kurudi nyuma katika sera hii kunaweza kuwa na gharama kubwa ya kisiasa kwa serikali yake.

Kwa mtazamo wa kimataifa, Uturuki inatuma ujumbe wa wazi kwa Magharibi na utawala vamizi wa Israel wa kutotetereka katika msimamo wake kuhusu Gaza. Nchi hiyo inaonyesha kwamba, haiko tayari kubadilisha sera zake kwa sababu ya mashinikizo kutoka kwa mataifa makubwa. Ankara inataka kuonyesha kwamba maamuzi yake yanafanywa kwa kuzingatia maslahi na kanuni zake, na sio kwa mujibu wa matakwa ya Washington au Tel Aviv.

Ni dhahiri shahiri kwamba, msimamo huu utairuhusu Uturuki kuimarisha uhalali wake wa kisiasa ndani na kutambuliwa kama taifa lenye ushawishi katika ngazi za kikanda na kimataifa. Mintarafu hiyo, kutupa kapuni msimamo huu si tu kwamba kunakinzana na sera na misingi iliyotangazwa ya serikali ya Erdogan, lakini pia kunaweza kudhoofisha nafasi ya nchi hiyo katika mahesabu na milingano ya kikanda na kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *