
M23 imeanza kujiondoa Jumatano kutoka mji wa Uvira mashariki mwa DR Congo, ambao ulianguka kwa kundi hilo la waasi wanaoungwa mkono na Rwanda katika shambulio la mapema Desemba ambalo liliikasirisha Washington.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Baada ya kuteka miji mikubwa ya Goma na Bukavu mapema mwaka huu, M23 iliteka mji huo wa kimkakati karibu na mpaka na Burundi siku ya Jumatano ya wiki iliyopita.
Kuiteka Uvira — mji wenye watu laki kadhaa — kuliiwezesha M23 kudhibiti mpaka wa ardhi na Burundi na kukata msaada wa kijeshi kutoka kwa jirani yake DRC.
Shambulio hili lilikuja siku chache tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya serikali za Kongo na Rwanda – makubaliano ambayo Rais wa Marekani Donald Trump aliyaita “muujiza mkubwa.” Hatua hii ililaaniwa vikali na Washington, ambayo iliahidi “hatua” kali kujibu “ukiukwaji mkubwa” wa makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani.
Siku ya Jumanne, M23 ilitangaza kwamba itajiondoa “kwa upande mmoja” kutoka Uvira kwa ombi la Marekani.
“Vikosi vyetu vimeanza kuondoka katika jiji la Uvira alasiri hii,” msemaji wa jeshi Willy Ngoma alibainisha siku ya Jumatano.
Vyanzo vya ndani na wawakilishi wa mahirika ya kiraia wameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanajeshi wa M23 wameanza kuondoka katika jiji hilo, wakielekea kaskazini, upande tofauti na shambulio lililoanzishwa mapema mwezi Desemba.
“Ninapozungumza nanyi, tunaona magari ya kijeshi ya M23 yakiondoka katika jiji hilo yakielekea kaskazini, labda kuelekea Luvungi,” mkazi mmoja amesema kwa simu.
“Niliwaona katika safu, wakiwa na mifuko yao ya kijeshi na silaha, wakielekea barabara kuu nambari 5,” barabara kuu ya eneo hilo, ambayo inapita kando ya mpaka wa Burundi kuvuka Bonde la Ruzizi, amesema mkazi mwingine.
“Hatujui watafika mbali kiasi gani… Inatia wasiwasi kidogo kwa sababu hatujui ni nani atakayehakikisha usalama wa jiji baada ya kuondoka kwa wapigaaji hao usiku wa leo,” wameongeza.
Walipowasiliana na AFP, kundi hili la waasi linalopinga serikali lilikataa kutaja kama wapiganaji au maafisa wa polisi wataendelea kubaki katika jiji hilo.
M23 iliwasihi “wapatanishi na washirika wengine kuhakikisha kwamba Uvira inalindwa kutokana na vurugu zote, kulipiza kisasi, na kurejesha waajeshi wa setikali na washirika wao,” amesema Bertrand Bisimwa, mkuu wa tawi la kisiasa, kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Kujiondoa “kutakamilika kesho,” ameongeza.
Msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya ametaka “kuwa macho” Jumatano jioni kujibu “madai ya kujiondoa” kwa M23 kutoka Uvira.
“Nani anaweza kuthibitisha hili? Wanaenda wapi? Wangapi walikuwepo? Wanaacha nini mjini? Makaburi ya halaiki? Wanajeshi waliojificha kama raia?” ameandika kwenye ùtandao wa kijamii wa X.
Waziri wa mambo ya nje wa Burundi alisiku iliyopita kwamba Rwanda “inajaribu tu kutuliza shinikizo la kimataifa.”
Ingawa Kigali haijawahi kukiri waziwazi kuunga mkono kundi hilo lenye silaha, Washington imeishutumu moja kwa moja Rwanda kwa kuhusika na kutekwa kwa Uvira na M23.
Siku ya Ijumaa Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, alilaani “ukubwa na ujanja” wa ushiriki wa Rwanda mashariki mwa DRC, akiishutumu kwa kupeleka wanajeshi hadi 7,000 katika eneo hilo.
M23 imekuwa ikikana uhusiano wowote na Rwanda na inasisitiza kwamba lengo lake ni kupindua serikali ya Rais wa Kongo Félix Tshisekedi.
Shambulio lake huko Uvira limesababisha vifo vya watu kadhaa, angalau 100 kujeruhiwa, na zaidi ya 200,000 kuhama makazi yao, kulingana na mashirika yasiyo ya kiserikali na Umoja wa Mataifa.
Angalau wakimbizi 85,000 wamekimbilia Burundi, ambapo wanaishi katika hali mbaya, kulingana na mamlaka ya Burundi.
Makubaliano ya amani yaliyosainiwa Washington yalilenga kukomesha miongo mitatu ya migogoro mashariki mwa DRC, eneo lenye utajiri wa madini. Yanajumuisha sehemu ya kiuchumi iliyoundwa ili kuhakikisha usambazaji wa madini muhimu ya Marekani yanayopatikana katika eneo hilo, huku Marekani ikijaribu kukabiliana na utawala wa China katika sekta hii.