Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu “kurejesha mikononi mwa nchi hiyo” ardhi na mafuta ya Venezuela yamefichua nia na sura halisi ya Marekani, na kusisitiza kuwa Washington haiwezi “kamwe” kuigeuza nchi hiyo ya Amerika Kusini kuwa “koloni” lake.

Akizungumza katika mkutano huko Caracas jana Jumatano, Rais Maduro amesema kuwa matamshi ya Trump yamedhihirisha namna Marekani inavyofanya kila iwezalo ili kubadili serikali halali iliyoko madarakani na kupora rasilimali za Venezuela.

“Ni kisingizio tu cha kuchochea vita na ukoloni, na tumesema mara nyingi, na sasa kila mtu anashuhudia uhakika wa mambo. Ukweli umefichuka na kubainika wazi”, amesema Rais wa Venezuela.

Rais Nicolas Maduro ameongeza kusema: Lengo la Marekani ni kubadili serikali nchini Venezuela na kuweka serikali kibaraka wake ambayo ingekabidhi utajiri wote wa nchi hiyo kwa Marekani na kuifanya Venezuela koloni lake lakini jambo hilo kamwe halitatokea. 

Siku ya Jumanne Rais wa Marekani alisema kuwa jeshi la Marekani litaendelea kujiimarisha karibu na Venezuela hadi hapo nchi hiyo itakaporejesha kile alichodai kuwa mafuta, ardhi na mali nyingine zilizoibwa kutoka Marekani. 

Itakumbukwa kuwa, mwaka 1970 Venezuela ilitaifisha sekta yake ya mafuta na hiyo kupunguza kwa kiasi kikubwa shughuli za makampuni ya Marekani katika sekta hiyo; makampuni ambayo awali yalikuwa yakijishughulisha pakubwa katika visima vya mafuta vya nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *