Mikoani. Wakati hali ya upatikanaji wa maji ikiendelea kuwa changamoto katika baadhi ya maeneo nchini kutokana na ukame, kwingineko wanalazimika kuchangia maji sehemu moja na mifugo.

Wapo wanaolalamikia kuuziwa maji kwa kwa gharama kubwa, kwa kuwa hayapatikani kwa urahisi kutokana na kuharibiwa kwa miundombinu, tatizo wanalosema limedumu kwa muda mrefu.

Kwa nyakati tofauti Mwananchi imetembelea maeneo ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Bahi, Mpwapwa, Chamwino na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro na kushuhudia baadhi ya wananchi na wafugaji wakihaha kutafuta majisafi na salama katika maeneo hayo.

Wakizungumza jana Jumatano, Desemba 17, 2025 na Mwananchi baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Meatu wamesema ukame unaoendelea umeathiri upatikanaji wa maji, hali inayowalazimu kutumia maji yasiyo salama kutoka kwenye mito na visima vya asili.

Wakazi wa kijiji cha Nyalanja Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye foleni kwa ajili ya kupata maji eneo hilo limekumbwa na ukame. Picha na Samwel Mwanga

Wananchi hao wamesema vyanzo vya miundombinu ya maji vinavyosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) vimekauka, hivyo kulazimika kutumia maji yasiyosafi na salama.

Mkazi wa Kijiji cha Nyalanja, Nghanga Mhoja amesema familia nyingi zenye watoto zinapitia wakati mgumu kutokana na kukosekana kwa huduma ya majisafi na salama na kwamba, zipo katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza.

“Tunalazimika kutumia maji ambayo hata mifugo inakunywa. Tunajua si salama lakini hatuna namna nyingine,” amesema Mhoja.

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Kimali, Asha Siloma amesema katika eneo hilo, wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita tano kutafuta maji ambayo hata hivyo, sio safi na salama.

“Tunatembea zaidi ya kilomita tano kufuata maji, lakini wakati mwingine hata hayo maji hatuyapati, tunarudi mikono mitupu kwa sababu mifugo imeyamaliza,” amesema.

Baadhi ya wakazi Njombe,  wakichota maji mto Kihesa kutokana na mgao wa maji uliopo baada ya mvua kuchelewa kunyesha mkoani humo. Picha na  Seif Jumanne

Amesema hali ya ukame imeathiri pia afya za mifugo yao iliyodhoofu kwa kukosa malisho na maji.

Akizungumzia changamoto hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Fauzia Ngatubura, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za dharura ikiwamo kubaini maeneo yenye maji kwa ajili ya uchimbaji wa visima ili wananchi pamoja na mifugo ipate huduma.

“Serikali inatambua changamoto hii na inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na mrefu ili kukabiliana na ukame unaojirudia,” amesema.

Hali ilivyo Dodoma

Sambamba na changamoto ya upatikanaji wa maji, wananchi wa  Bahi, Mpwapwa na Chamwino mkoani Dodoma, wamesema wanakabiliwa na uhaba wa malisho ya mifugo hali iliyosababishwa na ukame.

Mwenyekiti wa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo  Bahi, Ernest John amesema changamoto kubwa kwa sasa si uhaba wa maji bali ni upungufu wa malisho uliosababisha kushuka kwa bei ya mifugo.

“Maji siyo shida kubwa kwa sasa, lakini malisho ni tatizo kubwa. Ukame umeathiri sana wafugaji na bei ya mifugo imeshuka,” amesema.

Manyara shida ni ile ile

Akizungumza mmoja wa wafugaji wa kijiji cha Ogutu, Wilaya ya Simanjiro, Michael Oloishiye amesema kutokana na ukame, hali ya upatikanaji wa malisho na maji kwenye mabwawa imekuwa changamoto.

“Sisi wafugaji tunapata changamoto kubwa sana ya maji na mifugo yetu kukosa malisho na hali hii imefanya mifugo kudhoofu kwani mabwawa tuliyokuwa tukiyategemea yamekauka, hakuna tena maji,” amesema.

Mfugaji mwingine, Clemence Mollel amesema wafugaji hivi sasa wanalazimika kutembea na mifugo yao umbali mrefu zaidi ya kilomita 60 kufuata maji na malisho.

Wananchi wa Kata ya Mbokomu, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wanalazimika kutumia hadi Sh10,000 kwa siku kununua maji, hali inayochangiwa na uhaba wa huduma hiyo unaotokana na miundombinu chakavu na uharibifu wa mabomba.

Kwa sasa ndoo moja ya maji huuzwa kati ya Sh500 hadi Sh1,000 huku maji hayo yakisafirishwa kwa magari kutoka eneo la Kiboriloni, jambo linalowaathiri wananchi kiuchumi na shughuli zao za kila siku.

Diwani wa Mbokomu, Omben Massawe amesema tatizo hilo limekuwepo kwa muda mrefu na linachangiwa na miundombinu mibovu na ulegevu wa ulinzi wa mabomba ya maji.

“Maeneo mengi hayapati maji siyo kwa sababu ya upungufu wa vyanzo pekee, bali kutokana na uharibifu na wizi wa mabomba. Kuna maeneo maji hayafiki kabisa kwa sababu miundombinu imeharibiwa,” amesema Massawe.

Asha Shiloma mkazi wa kijiji cha Kimali Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu akichota maji katika kisima asili ambacho maji yake si safi na salama na hii inatokana na ukame katika wilaya hiyo. Picha na Samwel Mwanga

Amesema viongozi wa kata wameanza mipango ya kukutana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) na Ruwasa kupata ufumbuzi wa haraka.

Imeandikwa na Samuel Mwanga(Simiyu), Habel Chidawal(Dodoma), Joseph Lyimo(Manyara) na Florah Temba (Kilimanjaro).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *