
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ndiye ataongoza msafara wa Tanzania katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, mwaka huu hadi Januari 18, mwakani.
Hilo limethibitishwa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paramagamba Kabudi wakati alipotembelea kambi ya Taifa Stars nchini Misri.
“Tuna manaibu waziri wawili. Kuna mmoja ambaye mmeshamzoea, Mheshimiwa Mwinjuma (Hamisi) lakini pia sasa tuna Naibu Waziri wa pili, mheshimiwa Paul Christian Makonda na katika mechi hizi za AFCON Morocco tutakuwa na mheshimiwa Paul Christian Makonda,” amesema Kabudi.
Kabudi amesema kwamba Makonda ataungana na Taifa Stars kati ya Desemba 20 au 21 nchini Morocco.
Waziri Kabudi pia amewafikishia salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi la Taifa Stars na viongozi wa soka walioambatana na timu hiyo Misri.
Amesema kuwa Rais Samia amewatakia kila la kheri na anaamini watafanya vyema katika fainali hizo ambazo Taifa Stars imepangwa kundi C na timu za Uganda, Tunisia na Nigeria.
Pia Waziri Kabudi amewataka wachezaji kucheza kwa kujituma na kwa uzalendo wa hali ya juu ili timu hiyo ifike hatua za juu katika mashindano hayo.
Taifa Stars itacheza mechi ya kwanza ya AFCON 2025 dhidi ya Nigeria, Desemba 23, kisha Desemba 27 itacheza na Uganda na mechi ya mwisho itakuwa Desemba 30 dhidi ya Tunisia.