
Wakati zikibaki siku 11 kabla ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026 kuanzia, waandaaji wa mashindano hayo wamesema kutakuwa na ongezeko la timu nyingine mbili zitakazofanya idadi kamili iwe 10.
Awali ilitangazwa mashindano hayo yatashirikisha timu nane lakini kutokana na mvuto wake kwa awamu hii, waandaaji wa mashindano hayo wameamua kufanya timu shiriki ziwe 10.
Katibu wa mashindano Rashid Suleiman amesema kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika na sasa wanazisubiria timu.
“Kilichopo sasa ni kwamba, tumepokea maombi mengi ya timu zinazotaka kushiriki, hivyo kama kamati tunaangalia uwezekano wa kuongeza zisipungue kumi katika mashindano ya mwaka huu.
“Tunataka tuwe na makundi matatu ambayo yatazidi kuyafanya mashindano kuwa na mvuto zaidi.
“Wikiendi hii tunatarajia kutoa ratiba ya mashindano, hapo nd zitafahamika rasmi timu shiriki kwa mwaka huu.
“Ratiba hiyo itazingatia ushiriki wa Taifa Stars AFCON, hatutaki ingiliane ili kutoa nafasi kwa Watanzania kuishuhudia timu yao ikicheza ” amesema Rashid.
Kwa sasa timu nane ambazo zimethibitishwa kushiriki mashindano hayo ni Yanga, Simba, Azam, Singida Black Stars, Mlandege, Fufuni, KVZ na URA.
Bingwa wa mashindano hayo atapata Sh150 milioni na mshindi wa pili atapata Sh100 milioni.