MBUNGE wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, amewaomba wananchi wa Kisarawe na watanzania kwa ujumla kumuombea Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ana maono makubwa ya kuwatumikia Watanzania na kulisukuma Taifa mbele kimaendeleo.
Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kisarawe, kilicholenga kuwashukuru wajumbe kwa mchango wao katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuwashukuru kwa kuchaguliwa tena kuwa Mbunge wa jimbo hilo.
“Niwaombe wajumbe wa Halmashauri Kuu kuhakikisha tunamuombea Rais Dkt. Samia kwa kuwa ana kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo Watanzania na kuhakikisha Taifa letu linaendelea kusonga mbele,” amesema Dkt.Jafo
Ameongeza kuwa amani na usalama ni nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kumuombea Rais na Taifa kwa ujumla.
“Bila amani na usalama, nchi yetu haiwezi kupata mafanikio ya kiuchumi. Nawaomba wananchi wa Kisarawe na Watanzania kwa ujumla tuendelee kumuombea Rais wetu na Taifa letu, kwa sababu kiongozi wetu mwenye maono ni Rais Samia, na lazima tumuombee ili nchi yetu iendelee kusonga mbele,” amesema Dkt. Jafo
Awali, amesema baada ya ushindi huo, chama na serikali vimeanza rasmi awamu mpya ya kazi kwa kipindi cha miaka 5, huku akiendelea na utekelezaji wa majukumu ya maendeleo jimboni kupitia mkakati wao wa ‘Chaka kwa chaka’.
“Tumeanza kazi kwa mara nyingine katika msimu wa 2025–2030. Tumeendelea na kazi za jimboni, tukikutana na viongozi wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa, watendaji wa halmashauri, madiwani pamoja na wenyeviti wa vijiji na vitongoji vya Wilaya ya Kisarawe,” amesema Dkt. Jafo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kisarawe, Khalfan Sika, amesema jukumu la wanachama wa CCM ni kuipa ushirikiano Serikali ili kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi inatekelezwa kikamilifu.
“Ilani tuliyowapa Mhe. Rais, Mbunge na Madiwani ni Ilani ya CCM. Utekelezaji wake ndio mafanikio na suluhisho la kero za wananchi. Huu ni mkataba kati ya wananchi na CCM,” amesema.
Kadhalika, Mwenyekiti huyo amempongeza Dkt. Jafo kwa uungwana wake wa kukutana na Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchaguzi.
#StaeTvUpdate