
Merz: Ulaya lazima itumie mali za Urusi kumuongeza shinikizo Putin
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameutolea wito Umoja wa Ulaya kutumia mali za Urusi zilizozuiliwa kuisaidia Ukraine, “kuongeza shinikizo kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin” na “kutuma ishara ya wazi kwa Urusi.”
Kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unaofanyika leo mjini Brussels Tume ya Ulaya ilipendekeza mkopo wa yuro bilioni 90 kwa ajili ya Ukraine ili kuhakikisha hali ya kifedha ya nchi hiyo inaendelea kuwa thabiti kwa miaka miwili ijayo. Fedha hizo ni sehemu ya mali zenye thamani ya yuro bilioni 200 za Urusi zilizozuiliwa na Umoja huo.
Merz ameongeza kupitia mtandao wa X kwamba wananuia kuzitumia mali hizo za Urusi kufadhili Vikosi vya Ulinzi vya Ukraine kwa kama miaka miwili zaidi, lakini akatahadharisha kwamba hatua hiyo si kwamba inalenga kuviendeleza vita, na badala yake wanataka kuvimaliza vita hivyo haraka iwezekanavyo.
Hata hivyo, Merz na Tume ya Ulaya wanakabiliwa na vizingiti ndani ya Umoja wa Ulaya ambako wakuu wa mataifa washirika wa Urusi, Hungary na Slovakia tayari wamesema watapinga mipango kama hiyo. Jana Jumatano aidha, shirika la habari la AFP liliarifu kwamba Marekani nayo inayatilia shinikizo mataifa ya Ulaya kupinga mpango huo.
Muonyesheni Putin kwamba vita ‘havina maana,’ Zelenskyy auambia Umoja wa Ulaya
Katika hatua nyingine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewataka washirika wake kuionyesha Urusi kwamba vita vyake dhidi ya Kyiv havina maana yoyote. Amesema hayo kabla ya mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Ulaya. Zelensky amesema matokeo ya mikutano hiyo yanatakiwa kuifanya Urusi kuona hakuna maana yoyote ya kuendeleza vita hadi mwaka ujao kwa kuwa Ukraine itakuwa na uungwaji mkono.
Kulingana na Zelensky, Urusi inajiandaa na mwaka mwingine wa vita badala ya kuonyesha nia ya kuvimaliza vita hivyo, kama inavyodaiwa na Marekani.
Kwa upande wake Rais wa Urusi Vladimir Putin ameonya kwamba jeshi la nchi yake litaendelea kunyakua maeneo zaidi ya ikiwa Ukraine na washirika wake watayakataa masharti ya Moscow katika mazungumzo ya amani kati ya nchi hizo. Amesisitiza kuwa Urusi inataka kutumia diplomasia kushughulikia vyanzo vya mzozo, lakini kama Kyiv na washirika wake watakataa kushiriki mazungumzo ya kina, watalazimika kuikomboa ardhi yake ya kihistoria kwa mtutu wa bunduki.
Estonia yajenga mahandaki, ikijiimarisha kiulinzi dhidi ya Urusi
Huku hayo yakiendelea, Estonia imeanza kujenga mahandaki ikiwa ni sehemu ya hatua zake za kuimarisha ulinzi dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya Urusi hii ikiwa ni kulingana na kituo cha Uwekezaji wa Kiulinzi cha nchini humo. Kituo hicho kimesema maeneo 23 yatajengwa katika kipindi cha miezi ijayo, na ikitarajia kujenga mahandaki 600 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027, kwa ajili wanajeshi kujilinda dhidi ya kushambuliwa.