MLANDEGE ilimsajili kwa mbwembwe, Mshambuliaji Mfaransa, Enzo Claude Sauvage, lakini jamaa hakuanza katika mechi tisa za Ligi Kuu Zanzibar msimu huu kati ya 13 ilizocheza timu hiyo na siri imefichuka kuwa, mfumo ndio uliomfanya kukosa nafasi na kuondolewa mazima kikosini.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kucheza Wolverhampton Wanderers ya England upande wa vijana kuanzia mwaka 2017 hadi 2019, alitua Mlandege msimu huu na kufanikiwa kuanza katika mechi nne za kwanza za Ligi Kuu Zanzibar, baada ya hapo, amekosekana, huku ikifichuka kwamba ameondoka sambamba na nyota wengine wa kimataifa kikosini hapo.
Mbali na mechi hizo nne za ligi, pia alianza katika mechi tatu za Kombe la Kagame, akaanza tena Ligi ya Mabingwa Afrika zote mbili dhidi ya Ethiopia Insurance akifanikiwa kufunga bao moja, pia akaanza kwenye Ngao ya Jamii dhidi ya KMKM.
Enzo ni miongoni mwa wachezaji 13 waliosajiliwa na Mlandege msimu huu wakiwamo sita wa kigeni, huku mshambuliaji huyo akitarajiwa kuziba pengo la Abdallah Mtumwa ‘Pina’ aliyefunga mabao 21 Ligi Kuu Zanzibar msimu uliopita. Kwa sasa Pina anakipiga Pamba Jiji inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri China, amesema mfumo wa uchezaji unaotumika ndani ya kikosi hicho ndiyo sababu iliyomfanya Enzo kuamua kuondoka.
“Wachezaji wote waliotoka nje ya Tanzania wameshaondoka na hata alipokuwepo hakuwa na namba ya uhakika kwa namna ambavyo alikuwa anacheza,” amesema China.
Amesema, baada ya mchezaji huyo kuona hapati namba, ndio sababu ya kuamua kuondoka kwa lengo la kutafuta fursa upande mwengine, huku ikibainika kwamba Enzo aina yake ya uchezaji ni wa taratibu tofauti na mfumo wa timu wa kucheza kwa kasi.
Hata hivyo, Kocha Sabri amesema kuondoka kwake hakuna athari yoyote ndani ya timu kwani kikosi kinaendelea kufanya vizuri.
Mlandege ambayo ni watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, haikuanza vizuri msimu huu, lakini sasa imeanza kurudi kwenye ubora wake, huku Sabri akisema wanahitaji kulinda hadhi ya timu hiyo na kutetea ubingwa.
Amesema hamasa na morali kwa wachezaji imeanza kurudi kwa kiasi kikubwa baada ya kupitia kipindi kigumu.
Akizungumzia ushindi wa juzi dhidi ya KVZ wakishinda 1-0, amesema ni kama wamelipa kisasi kwani mara ya mwisho walipokutana msimu uliopita 2024-2025 walipoteza kwa idadi kama hiyo.
“Sasa naanza kuiona Mlandege ile niliyokuwa nikiitaka, tutajipanga kuhakikisha tunafika tunapohitaji,” amesema Sabri.
Wachezaji wa kimataifa waliotua Mlandege msimu huu ni Vitor De Souza na Davi Nascimento (Brazil), Hamis M’sa na Alphonce Ahmed (Comoro), Fortune Chidera (Nigeria), Ishamel Robino (Ghana) na Enzo Claude Sauvage (Ufaransa).
Katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar, Mlandege inashika nafasi ya saba ikikusanya pointi 21, ikishinda mechi tano, sare sita na kupoteza mbili huku ikifunga mabao 17 na kuruhusu sita.
MECHI ALIZOANZA
KMKM 0-0 Mlandege
Mlandege 0-0 JKU
Polisi 1-0 Mlandege
Mlandege 0-0 Mafunzo
MECHI ALIZOKOSEKANA
New Stone Town 0-3 Mlandege
Fufuni 0-2 Mlandege
Mwembe Makumbi 0-0 Mlandege (alikaa benchi)
Mlandege 0-0 Zimamoto
Mlandege 2-0 Malindi
Uhamiaji 2-2 Mlandege
Mlandege 6-1 Junguni
Mlandege 0-2 Chipukizi
Mlandege 1-0 KVZ