Msanii maarufu wa muziki wa Bongofleva wenye ladha ya R&B na Afro-pop, Christian Bella amepewa uraia wa Tanzania
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene leo Alhamisi, Desemba 18, 2025 ikiwa ni siku ya wahamaji duniani.
Simbachawene amesema Tanzania kuna idadi kubwa ya wahamiaji na baadhi yao wamekuwa wakipewa uraia.
“Sasa anakwenda wapi, amekwisha fika, ameoa hapa, ana watoto hapa na atapata wajukuu hapa. Anafanya kazi vizuri, hana makosa, amefuata utaratibu na muda wote alioishi hapa amelipa malipo stahiki, siyo wengine wanaolanda landa tu,” amesema Simbachawene.
Amesema mtu anaweza kupewa uraia na ukafutwa kama hatafuata utaratibu: “Hatuwezi kumpa uraia mtu ambaye ni hatari ama anayegeuka kuwa hatari, kwa hiyo kuna ‘vetting’ imefanyika kabla ya mtu kupewa uraia.”
Awali, Bella alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambaye ameishi Tanzania kwa muda mrefu akifanya shughuli za kisanii.
Christian Bella aliingia Tanzania kati ya mwaka 2006 hadi 2009. Alikuja nchini kutokana na changamoto za kisiasa na kiuchumi zilizokuwa zikiathiri sekta ya muziki nchini kwao, hali iliyomfanya kutafuta fursa mpya za kuendeleza kipaji chake.
Tanzania ilimpa mazingira mazuri ya kukuza muziki wake na hatimaye akapata umaarufu mkubwa ndani ya nchi hiyo y Afrika mashariki.
Akiwa Tanzania, Christian Bella alianza kufanya kazi na bendi ya Akudo Impact, ambayo ndiyo iliyomsaidia kutambulika kwa haraka kupitia nyimbo zake zilizopendwa na mashabiki wa muziki wa dansi, hususan wimbo “Walimwengu Si Binadamu.”
Baada ya kupata uzoefu na umaarufu, alijitenga na bendi hiyo na baadaye akaanzisha bendi yake mwenyewe iitwayo Malaika Music Band, ambayo imekuwa chini ya usimamizi wake na imechangia sana katika safari yake ya muziki.
Kwa ujumla, Christian Bella amefanya kazi na bendi kuu mbili akiwa Tanzania, ambazo ni Akudo Impact na Malaika Music Band. Kupitia bendi hizo, pamoja na ushirikiano na wasanii mbalimbali wa Tanzania na Afrika kwa ujumla, ameweza kujijenga kama mmoja wa waimbaji wakubwa wa muziki wa dansi na rumba nchini Tanzania.