MSHAMBULIAJI na nahodha wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, John Bocco ‘Adebayor’ ametajwa kurudishwa tena Msimbazi kwa lengo la kuongeza nguvu benchi la ufundi la timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Bara na iliyopo makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nyota huyo wa zamani wa Kijitonyama Rangers, Cosmopolitan na Azam FC, msimu uliopita alikuwa JKT Tanzania aliyojiunga nayo baada ya kumaliza mkataba na Wekundu wa Msimbazi na kuifungia mabao mawili, kabla ya kudaiwa amejikita kwenye ishu na ukocha aliouanza tangu akiwa Simba.

Hata hivyo, taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni kwamba, Bocco aliyeitumikia Simba kwa mafanikio inaelezwa anarudi kama kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili yaani fitness coach ili kusaidiana na Mohammed Mrishona ‘Xavi’.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa Bocco kimeliambia Mwanaspoti, Simba ipo katika mazungumzo na mshambuliaji huyo wa zamani ili kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi la timu hiyo.

“Xavi hana msaidizi na sasa yupo timu ya taifa, yamefanyika mapendekezo na kupitishwa jina la Bocco kuwa sehemu ya kocha aliyeongeza nguvu kwa kusaidiana na kocha huyo atakaporejea kutoka kwenye majukumu ya kitaifa,” amesema na kuongeza;

“Mazungumzo na mshambuliaji huyo ambaye tayari amepata kozi ya mazoezi ya utimamu wa mwili tunaamini ataweza kuwa sehemu ya mafanikio kwa kuiweka timu katika hali ya utimani kwani ni mzoefu na anafahamu mifumo mingi ya timu.”

Mtoa taarifa huyo amesema Bocco ataungana na timu mapema itakaporejea kambini kwa lengo la kuendelea pale ilipoishia timu na mara baada ya Xavi kurudi wataunganisha ngumu na kuwa sehemu moja ya kuitoa timu ilipo na kuifikisha kwenye malengo.

Wakati ikitajwa Bocco kurudi Simba Mwanaspoti linafahamu mshambuliaji huyo mwenye rekodi ya kuwa Mfungaji Bora wa muda wote wa Ligi Kuu akiwa na mabao 156 alikuwa timu ya vijana ya U20 ya JKT Tanzania akisimama kama kocha mkuu wa timu hiyo.

Pia kabla ya kumaliza mkataba na Simba uongozi wa timu hiyo ulikuwa na mpango wa kumstaafisha ili aweze kusomea ukocha hilo lilishindikana, kwani alipata ofa ya kuitumikia JKT Tanzania kwa msimu mmoja baada ya hapo ndipo alipoingia darasani kusomea ukocha.

Endapo dili lake litaenda kama lilivyopangwa yeye kutua Simba basi mkakati wa Simba kuendeleza wachezaji waliopita kwenye timu hiyo utaendelea baada ya Suleiman Matola aliyepo hapo tangu mwaka 2019.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *