
Russia imefanya mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Ukraine kwa muda wa masaa kadhaa ambapo miripuko mikubwa imesikika huko Kyiv na miji mingine ya nchi humo.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko, ametangaza habari hiyo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram na kuandika kwamba, mifumo ya ulinzi wa anga katika wilaya ya Obolonsky (moja ya wilaya za kaskazini mwa mji mkuu wa Ukraine) imekabiliana na mashambulizi hayo kwa muda mrefu.
Naye gavana wa mkoa wa Sumy, Oleh Hryurov, amesema kuwa, shambulio kubwa la droni za Russia limefanyika kwenye mkoa huo na kwamba mashambulizi hayo yalilenga miundombinu ya nishati na kusababisha kukatika kwa wingi umeme katika eneo hilo.
Naibu Waziri wa Nishati wa Ukraine, Mykola Kolesnik pia ametoa taarifa ya kukatika umeme katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Donetsk.
Oleh Kiper, gavana wa mkoa wa Odessa wa kusini mwa Ukraine, pia ametangaza katika ujumbe wake kwenye Telegram kwamba, mashambulizi makubwa ya Russia dhidi ya vituo vya umeme na vituo vya nishati katika eneo hilo yamesababisha kukatika umeme kwa familia 280,000. Ameongeza kuwa, umeme wa nyumba 220,000 umerejeshwa, lakini mtandao bado umeharibika na unahitaji matengenezo makubwa.
Wakati huo huo waungaji mkono wa Russia huko Zaporozhye wametangaza kwamba kiwanda cha nyuklia cha eneo hilo hivi sasa kinaendeshwa na waya mmoja tu badala ya miwili kutokana na sababu za kijeshi, suala ambalo ni hatari kwa usalama wa raia.