
WAKATI uongozi wa Singida Black Stars ukitafuta beki mwingine wa kati, majina ya nyota wawili yamewekwa mezani, ambayo ni Abdallah Kheri ‘Sebo’, anayeichezea kwa sasa Pamba Jiji kwa mkopo akitokea Azam na Abdulmalik Zakaria wa Mashujaa.
Mabosi wa Singida wanapambana kuongeza beki mwingine wa kati, baada ya kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi kumtumia zaidi kiungo mkabaji, Morice Chukwu, licha ya uwepo pia wa nyota wengine wakiwamo, Anthony Tra Bi Tra na mzawa, Kennedy Juma.
Tra Bi Tra aliyejiunga na Singida Julai 8, 2024, akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, amekuwa muhimili mkubwa wa kikosi hicho tangu aliposajiliwa, licha ya Mnigeria Morice Chukwu kuchezeshwa mara kwa mara eneo hilo tofauti na kiungo.
Mwanaspoti limepata taarifa, miongoni mwa mabeki wazawa wanaofuatiliwa kwa sasa ni Sebo anayeichezea Pamba kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Azam ambao kwa sasa umebakia miezi sita, kama ilivyo pia kwa beki wa Mashujaa, Abdulmalik Zakaria.
Sebo aliyetamba na timu za JKU, Zimamoto na Ndanda, baada ya msimu huu kuisha atakuwa amemaliza mkataba wake na Azam, hivyo atakuwa huru kusaini kokote, jambo linaloipa nguvu Singida kuanza kumfuatilia kwa ukaribu ili kuipata saini yake.
Kwa upande wa Abdulmalik aliyejiunga na Mashujaa akitokea Namungo Julai 19, 2024, anamaliza pia mkataba wake na maafande hao mwisho wa msimu huu, licha ya uongozi wa kikosi hicho kuanza tena mazungumzo kwa ajili ya kuongeza kandarasi mpya.
Mwanaspoti linajua Singida inataka kumrejesha beki Mghana Frank Assinki aliye Yanga kwa mkopo.
Assinki aliyejiunga na Singida Desemba 24, 2024, akitokea Inter Allies ya kwao Ghana, ameshindwa kushindania nafasi na nyota wenzake, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Bakari Mwamnyeto, hivyo, huenda akarudi katika dirisha hili dogo.