RAIS wa Marekani, Donald Trump, amelihutubia taifa leo Alhamisi, akieleza mipango yake ya kuifanya Marekani kuwa imara zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Katika hotuba yake, Rais Trump aliorodhesha kile alichokitaja kuwa mafanikio ya mwaka wake wa kwanza madarakani, akisema alirithi nchi ikiwa katika hali mbaya kutoka kwa mtangulizi wake, Joe Biden, lakini ameweza kuleta mabadiliko makubwa kuliko rais mwingine yeyote katika historia ya Marekani.
Amedai kuwa sera za chama cha Democratic zilichangia kupanda kwa bei ya vyakula, lakini akasisitiza kuwa serikali yake tayari inachukua hatua za kutatua changamoto hiyo. SOMA: Mawakala 120 Marekani wavutiwa utalii Tanzania
“Mtaona mabadiliko hayo katika pochi zenu na akaunti zenu za benki katika mwaka mpya. Baada ya miaka mingi ya mapato kushuka kwa viwango vya kihistoria, sera zetu sasa zinaongeza mshahara unaobaki mikononi mwa wafanyakazi kwa kasi ya kihistoria.
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, mishahara inaongezeka kwa kasi kubwa zaidi kuliko mfumuko wa bei,” alisema Rais Trump. Pia amegusia masuala ya uhalifu, uhamiaji, vita dhidi ya dawa za kulevya pamoja na juhudi za kuliimarisha upya jeshi la Marekani.
Katika mipango yake ya baadaye Rais Trump amepanga kupunguza gharama za maisha, linaloibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa Wamarekani, huku akiahidi kuwa uchumi wa taifa hilo utaimarika kwa kiwango kikubwa mwaka ujao, akisema dunia haijawahi kushuhudia kiwango kama hicho cha ukuaji wa kiuchumi.
