Donald Trump alianza hotuba yake kwa kuushambulia utawala wa mtangulizi wake, Joe Biden, akisema kuwa miezi 11 iliyopita aliirithi nchi ikiwa katika kile alichokiita mparaganyiko, taifa likiwa katika hali mbaya ya kiuchumi na kiutawala. Alisema anaendelea kurekebisha uharibifu uliosababishwa na serikali iliyopita, akisisitiza kuwa hali hiyo si kosa lake.
“Jioni njema Marekani. Miezi 11 iliyopita, nilirithi hali mbaya na sasa nairekebisha. Nilipoingia madarakani, mfumuko wa bei ulikuwa mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 48. Katika historia ya nchi yetu, jambo hilo liliifanya bei za bidhaa kupanda kuliko muda mwengine wowote na kufanya hali kuwa ngumu kwa mamilioni na mamilioni ya wamarekani.”
Rais huyo alikuwa akijibu hasira za wapiga kura wanaolalamikia kupanda kwa gharama za maisha. Donald Trump aliendelea kuushambulia utawala wa Biden kwa takriban dakika 20 za hotuba yake. Licha ya malalamiko hayo, Trump alisema serikali yake imeleta mabadiliko chanya kuliko rais yeyote katika historia ya Marekani. Baada ya hapo, aliweka wazi mipango ambayo alisema itaifanya Marekani kuwa imara zaidi kuliko hapo awali.
Trumpa asifia hatua serikali yake inayochukua dhidi ya uhamiaji
Rais huyo bilionea mwenye umri wa miaka 79, alitumia pia sehemu kubwa ya hotuba yake, kusifia hatua anazosema serikali yake inachukua dhidi ya uhamiaji.
Akitaja juhudi za kuimarisha ulinzi wa mipaka ya Marekani, Trump alitetea sera ya kuwarejesha nyumbani wahamiaji, akidai kuwa serikali yake inawaondoa wahalifu nchini humo. Aliushambulia tena utawala wa Biden kwa madai kuwa uliruhusu zaidi ya watu milioni 25, kuingia nchini Marekani akiwalenga wahamiaji, ingawa takwimu hizo zimekuwa zikitiliwa shaka na wachambuzi.
Kwa mujibu wa takwimu zinazotajwa na wataalamu, takriban wahamiaji milioni 7.4 wasio na vibali halali waliingia nchini Marekani chini ya utawala wa Biden. Katika hotuba yake, Trump pia alisema bei za nishati, ikiwemo gesi na mafuta, zimekuwa zikishuka—madai ambayo baadhi ya Wamarekani wanasema sio sahihi. Aidha, alitangaza malipo ya zaidi ya dola 1,776 kama bonasi ya Krismasi kwa wanajeshi takriban milioni 1.5.
Wachambuzi: Alichokisema Trump na uhalisia uliopo sio sawa
Hata hivyo, swali linalobaki kwa wengi ni iwapo hotuba ya Trump imejibu matarajio ya Wamarekani au imejikita zaidi katika kuulaumu utawala uliopita. Mubelwa Bandio, mchambuzi wa siasa anayeishi Marekani, anaeleza:
“Vitu vingi vilivyogusiwa mule ndani, havina ukweli. Alizungumzia kuhusu kushuka kwa bei lakini, taarifa kutoka katika serikali yake inaonesha kwamba bei ya vyakula iko juu kwa zaidi ya asilimia 3. Ni kweli kwamba mafuta imeshuka lakini vyote vingine vimepanda. kwa watu wengi alichokizungumzia na uhalisia uliopo sio sawa.”
Miongoni mwa masuala aliyoyagusia kwa ufupi ni vita dhidi ya dawa za kulevya na juhudi za kuimarisha upya jeshi la Marekani. Trump pia ameahidi kuwa Marekani itaimarika kiuchumi mwaka ujao kwa kiwango ambacho dunia haijawahi kushuhudia.