TUZO za Oscar zitaanza kuonyeshwa mubashara kupitia YouTube kuanzia mwaka 2029, baada ya kampuni ya teknolojia kushinda zabuni ya haki za utangazaji dhidi ya watangazaji wengine.
Kwa zaidi ya miongo mitano, sherehe hizo zimekuwa zikirusha matangazo yake kupitia kituo cha televisheni cha Marekani, ABC, tangu miaka ya 1970. Tuzo za Oscar, zinazochukuliwa kuwa tukio kubwa zaidi katika tasnia ya filamu duniani, zitapatikana bure kwa zaidi ya watumiaji bilioni mbili wa YouTube kote ulimwenguni.
Hata hivyo, watazamaji waliopo Marekani watalazimika kuwa na usajili wa YouTube TV ili kutazama matangazo hayo mubashara. Makubaliano hayo yataendelea hadi mwaka 2033 na yanajumuisha haki za kuonyesha matukio yote muhimu, ikiwemo matembezi ya zulia jekundu, hafla nzima ya utoaji tuzo pamoja na tamasha la Governors Ball.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, hatua hiyo inalenga kufanya Tuzo za Oscar zipatikane kwa urahisi zaidi kwa hadhira ya kimataifa inayozidi kuongezeka, kupitia vipengele vya kisasa kama vile nyimbo za sauti na maandishi ya manukuu katika lugha mbalimbali. SOMA: Filamu “No Other Land” yashinda Oscar
