
Ripoti iliyotolewa Alkhamisi na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema zaidi ya raia 1,000 waliuawa wakati kundi la waasi wa Sudan lilipotwaa udhibiti wa kambi ya wakimbizi wa ndani huko Darfur nchini Sudan mwezi Aprili mwaka huu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, kwa miezi kadhaa kabla ya shambulio la Aprili 11-13, Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF vilizuia kuingia kwa chakula na vifaa kwenye kambi ya Zamzam katika eneo la magharibi mwa Sudan la Darfur, makazi ya karibu watu nusu milioni waliokimbia makazi yao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Wakati wa kuchukua udhibiti, RSF ilielekeza mashambulizi dhidi ya raia, na manusura waliripoti kujiri mauaji, ubakaji, mateso na utekaji nyara, huku kwa akali watu 319 wakiuawa kambini au walipojaribu kukimbia,” imeeleza ripoti hiyo.
“Mauaji hayo ya makusudi ya raia yanaweza kuwa uhalifu wa kivita,” amesema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk katika taarifa iliyoambatana na ripoti hiyo ya kurasa 18.
Mmoja wa mashuhuda anasema kwamba, watu wanane waliokuwa wamejificha katika chumba kambini waliuawa na wapiganaji wa RSF ambao walipenyeza bunduki kupitia dirishani na kuwafyatulia risasi wakimbizi hao, ripoti hiyo imesema.
Pande mbili za Jeshi la Sudan, SAF na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF zimekuwa zikipigana vita tangu Aprili 2023 ambavyo vimeua zaidi ya watu 20,000 na kuwafanya wengine milioni 14 walazimike kuyahama makazi yao.
Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Hata hivyo utafiti wa vyabnzo vingine huru unakadiria idadi ya vifo kuwa ni karibu 130,000.