
Wahamiaji thelathini na wawili wa Bangladesh wameokolewa baada ya boti yao kuzama katika pwani ya mji wa Al-Haniya wa kaskazini mashariki mwa Libya.
Tawi la Al-Jabal Al-Akhdar la Shirika la Kupambana na Uhamiaji Haramu la Libya limetangaza habari hiyo na kuripoti kwamba wahamiaji wote waliokuwemo ndani ya chombo hicho wameokolewa na kuhamishiwa katika kituo cha mapokezi na ambapo ni aina fulani ya kuwekwa kizuizini huko Al-Bayda. Wakiwa kizuizini, Wabangladesh hao wamepewa huduma ya kwanza na muhimu ya kimatibabu. Baadhi ya wahamiaji hao walikuwa wamepata majeraha madogo wakati wa hekaheka za kupambana na mawimbi makali ya baharini.
Shirika la Kupambana na Uhamiaji Haramu la Libya limesema kwamba tukio hilo limesababishwa na hali mbaya ya hewa.
Taarifa hiyo pia imeonya kuhusu hatari za kuongezeka wimbi la uhamiaji usio wa kawaida baharini, ikielezea kile kinachoitwa “boti za kifo” kuwa ni tishio kubwa kwa maisha ya binadamu, hasa wakati hali ya hewa inapokuwa mbaya na mawimbi ya maji yapokuwa makubwa baharini.
Libya kwa muda mrefu imekuwa kitovu kikubwa cha usafiri kwa wahamiaji wasio wa kawaida kutokana na nchi hiyo kuwa katika eneo muhimu la kijiografia na kuwa karibu kwake na bara Ulaya. Libya ina fukwe ndefu za Bahari ya Mediterania.
Tangu ulipoangushwa utawala wa kiongozi wa zamani Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya imeshindwa kuwa na utulivu na hakuna serikali yenye nguvu nchini humo, suala ambalo limeruhusu Libya kuvamiwa na mitandao ya magendo na kufanya kazi zao kwa uhuru.