Wakati michuano ya AFCON 2025 ikianza wikiendi hii nchini Morocco, je unawafahamu baadhi ya ndugu na mapacha waliowahi kuchezea timu zao za taifa kwenye mashindano hayo?
Ndugu wawili kutoka familia ya Toure; nawazungumzia Kolo na mdogo wake Yaya, waliwasaidia Tembo wa Ivory Coast kufika fainali ya AFCON mwaka 2006, 2012 na kutwaa kombe hilo mwaka 2015 nchini Equatorial Guinea.
Ndugu hao wawili wameshiriki jumla ya michuano sita ya AFCON wakiwa na timu ya taifa ya Ivory Coast.
Nadhani unamkumbuka Abedi Pele, yule gwiji wa soka kutoka Ghana.
Abedi Ayew Pele, alikuwa na watoto watatu; Andre, Ibrahim pamoja na Jordan Ayew ambao waliiwakilisha Ghana kwenye michuano ya AFCON.
Kwa miaka 13, Andre Ayew na ndugu yake Jordan, wameiwakilisha Black Stars ya Ghana kwenye michuano ya AFCON, licha ya kutobeba kombe hilo.
Ndugu hao wanakumbukwa zaidi kwa ushirikiano wao uwanjani, hasa wakati wa fainali za mwaka 2012 zilizofanyika Equatorial Guinea na Gabon, ambapo Ghana ilipoteza kwa Zambia kwenye hatua nusu fainali.
Kabla ya hapo, waliwahi pia kucheza pamoja na ndugu yao aitwaye Ibrahim Ayew, kwenye AFCON ya mwaka 2010.
Wakijulikana kwa muonekano wa vipara vyao ving’aavyo, Ibrahim Hassan na pacha wake walijipatia umaarufu mkubwa, wakati wakiwachezea mafarao wa Misri.
Wakati Hossam akikumbukwa kuwa uhodari wake wa kufunga magoli, Ibrahim alijulikana zaidi katika nafasi ya ulinzi.