Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 10
Katika miaka ya hivi karibuni, Afrika imeshuhudia kuibuka kwa wanawake wengi wanaoshika nafasi za kufanya maamuzi.
Ingawa uwakilishi wao bado hauko sawa katika nchi kadhaa, ushawishi wao iwe katika makampuni makubwa, taasisi za kimataifa au katika uongozi wa kisiasa barani unabaki kuwa mkubwa.
Miongoni mwa haiba hizi za wanawake, nje ya siasa, kuna wale wanaojitofautisha katika fedha, sayansi, tasnia, teknolojia au mitindo.
Wao ni mifano ya kuigwa na chanzo cha ushawishi kwa viongozi wanawake wa kesho barani Afrika.
Mwaka 2025 pia uliadhimishwa kwa mafanikio ya wanawake hawa, ambao ushawishi wao umevuka mipaka ya Afrika.
Njia yao ya taaluma ni ya kuvutia, ikichangiwa na msukumo wa kuwajibika na dhamira isiyo na kifani kwa bara Afrika; uwezo wao wa kubadilisha sekta zao kwa matokeo makubwa katik akipindi kifupi, wanawake hawa wameonyesha kuwa wanaweza kuongoza miradi nyeti na ya kimkakati ili kuinua Afrika zaidi.
Mienendo na mabadiliko haya yote yanayoendeshwa na wanawake yanavutia kote barani na kuwaweka mbele ya kamera wakivutia kwa kupitia kazi zao.
Marais wa Jamhuri, Mawaziri Wakuu, marais wa taasisi, viongozi wa makampuni mashuhuri, hawa hapa wanawake kumi (10) walioadhimisha mwaka wa 2025 katika bara la Afrika.
1. Bella Disu, nyota wa teknolojia
Chanzo cha picha, Bella Disu/Instagram
Belinda Ajoke Olubunmi Adenuga, anayejulikana kama Bella Disu, ni mjasiriamali na kiongozi wa Nigeria mwenye sifa nzuri ya uvumbuzi katika sekta za mawasiliano ya simu, mali isiyohamishika, na uhisani.
Mkurugenzi mtendaji wa Globacom na Mkurugenzi Mtendaji wa Cobblestone Properties, mwanamke huyu kijana, mwenye umri wa miaka 40 tu, ni mdau muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Nigeria, kwa mujibu wa orodha ya Africa Business Index, ikinukuu Forbes Africa.
Pia anahudumu katika bodi za Julius Berger Nigeria Plc na Abumet Plc, kampuni mbili zilizobobea katika ujenzi na utengenezaji wa vioo na usindikaji wa alumini.
Akiwa na umahiri mkubwa katika majadiliano ya mikataba na usimamizi wa miradi mikubwa yenye athari za hali ya juu, ameongoza mipango kadhaa ya kiwango kikubwa, ikiwemo makazi ya kifahari ya “Sisi Paris”, “Ile Oja Shopping Mall”, pamoja na Alliance Française Mike Adenuga, kituo cha kitamaduni kilichozinduliwa mwaka 2018 na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.
Bella Disu pia ni mfadhili mwenye kujitolea kwa jamii. Kupitia Bella Disu Foundation (BDF), anajitahidi kuboresha hali za maisha za jamii nyingi nchini Nigeria.
Aidha, akiwa mwandishi katika muda wake wa ziada, alichapisha kitabu cha watoto mnamo Juni 2022 kiitwacho Soso and the Kako Leaf, ambacho kilimletea Tuzo ya Gold Mom’s Choice pamoja na ukadiriaji wa nyota tano kutoka Readers’ Favorite.
Mnamo mwaka 2019, serikali ya Ufaransa ilimtunuku heshima ya juu ya Knight of the Order of Arts and Letters.
Hivi karibuni zaidi, mnamo Machi 2025, Forbes Africa ilimjumuisha miongoni mwa wanawake 50 wa Kiafrika wanaoshikilia nyadhifa za juu katika sekta ya uchumi.
Pia alitunukiwa na Gavana Sanwo-Olu kupitia mpango wa “Lagos Eko 100 Women”, na akatajwa katika orodha ya Choiseul 100 Africa ya miaka 2022 na 2023, inayowatambua watu wanaounda mustakabali wa uchumi wa bara.
Kwa kuzingatia safari yake ya taaluma, Bella Disu anajitokeza kama chanzo kikubwa cha msukumo kwa wanawake vijana barani Afrika, leo na kwa vizazi vijavyo.
2. Netumbo Nandi-Ndaitwah, mwanaharakati aliyejitolea kuongoza nchi
Chanzo cha picha, Getty Images
Kuibuka kwa mwanamke huyu wa Namibia kunaonyesha mabadiliko yanayotokea katika siasa za Afrika, ambapo wanawake wengi zaidi wanapata nafasi za juu zaidi za serikali.
Netumbo Nandi-Ndaitwah pia ni miongoni mwa wanawake 50 wenye ushawishi mkubwa barani Afrika, kulingana na Forbes Africa.
Alikuwa ishara yenye nguvu ya uongozi wa kike wa Kiafrika alipochaguliwa kuwa Rais wa Namibia mnamo Machi 21, 2025, na kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza nchi hii ya kusini mwa Afrika.
Akiwa na umri wa miaka 73, yeye ni miongoni mwa wakuu wa Shirika la Watu wa Kusini Magharibi mwa Afrika (SWAPO), harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Afrika Kusini ambazo zilikuwa chama tawala cha siasa baada ya uhuru mwaka wa 1990.
Akipewa jina la utani “NNN”, alikuwa akijituma zaidi katika Komsomol – shirika la vijana la Chama cha Kikomunisti cha Soviet – wakati wa uhamisho wake nchini Urusi miaka ya 1970.
Pia mdumisha uhusiano wa kihistoria na Korea Kaskazini, ambayo inahusika katika miradi kadhaa nchini Namibia.
Mhafidhina, anatetea sheria kali kuhusu utoaji mimba, isipokuwa katika matukio ya kipekee.
Baada ya kuhudumu bungeni miaka ya 1990, alijiunga na serikali.
Mwaka 2000, akawa Waziri wa Wanawake na Watoto, kabla ya kushikilia wizara ya mambo ya kigeni kwa miaka kumi na miwili (2012-2024).
Alichaguliwa katika uchaguzi wa Februari 2025, Netumbo Nandi-Ndaitwah sasa anaongoza nchi yenye wakazi milioni 3, 70% yao wakiwa chini ya umri wa miaka 34, kulingana na sensa ya 2023.
3. Kate Fotso, kiongozi aliyethibitishwa katika sekta ya kilimo na chakula
Chanzo cha picha, Getty Images
Kate Fotso, mtu tajiri zaidi wa 20 katika nchi zinazozungumza Kifaransa Afrika na mwanamke wa kwanza kuonekana katika nchi 30 tajiri zaidi zinazozungumza Kifaransa Afrika, ni mfanyabiashara mwanamke aliyefanikiwa kutoka Cameroon.
Mkurugenzi Mtendaji wa Telcar Cocoa Ltd yenye makao yake makuu nchini Cameroon, kampuni yake imekuwa kampuni kubwa zaidi ya kuuza nje kakao kwa zaidi ya miaka thelathini, ni kiongozi katika uwanja huo akiwa na zaidi ya 30% ya kiasi cha mauzo ya nje na mfanyabiashara wa kampuni ya Marekani ya Cargill.
Rais wa Muungano wa wauzaji wa Kakao Cameroon, Bi. Fotso pia yuko kwenye bodi ya wakurugenzi ya kampuni kadhaa na ana utajiri unaokadiriwa kuwa dola milioni 252 au takriban FCFA bilioni 150 kwa mujibu wa Forbes Africa.
Kampuni yake imesambaza FCFA bilioni 1.5 kwa wazalishaji wa kakao walioidhinishwa katika misimu mitatu iliyopita ya kakao.
Telcar Cocoa ilishika nafasi ya 18 kati ya kampuni 100 bora za Cameroon katika suala la mapato.
Telcar Cocoa imejitolea kwa masuala ya maendeleo endelevu na Kate Fotso anasifiwa kwa uongozi wake katika sekta ya kilimo na chakula.
4. Nialé Kaba, mtu mashuhuri katika uchumi wa Ivory Coast
Chanzo cha picha, Getty Images
Anachukuliwa kuwa mbunifu wa mipango ya kiuchumi ya Côte d’Ivoire tangu alipojiunga na serikali ya nchi yake mwishoni mwa mgogoro wa baada ya uchaguzi wa mwaka 2010.
Nialé Kaba ni miongoni mwa wanawake wachache waliodumu kwa muda mrefu katika nyadhifa za juu za uwaziri.
Ni mwanamke mwenye kujisitiri, lakini anadhihirisha nidhamu na umakini mkubwa katika usimamizi wa uchumi, jambo linaloonekana kupitia takwimu zinazoendelea kuimarika.
Kwa mujibu wa Wizara ya Uchumi, Mipango na Maendeleo ya Côte d’Ivoire, ametekeleza mageuzi ya kiuchumi na kifedha yaliyoimarisha mfumo mkuu wa uchumi (macroeconomic framework) na kurejesha imani ya wawekezaji binafsi pamoja na washirika wa maendeleo.
Chini ya uongozi wake, Côte d’Ivoire ilifanikiwa kupata viwango vya mikopo (credit ratings) kutoka taasisi mashuhuri za kimataifa za Moody’s na Fitch, na kufanya jitihada zake za kwanza za kukusanya mitaji katika masoko ya fedha ya kimataifa.
Katika kipindi hicho, uchumi wa nchi ulirekodi wastani wa ukuaji wa asilimia 9% kwa mwaka, na kuifanya iwe miongoni mwa uchumi wenye kasi zaidi barani Afrika.
Ana ujuzi wa hali ya juu katika mazungumzo, na ni Gavana wa Côte d’Ivoire katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Uwekezaji na Maendeleo ya ECOWAS (EBID), pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IsDB).
Nialé Kaba, ambaye aliorodheshwa na Forbes Africa miongoni mwa wanawake 50 wenye ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika, ameongoza pia makongamano kadhaa ya kimataifa kuhusu uchumi na maendeleo.
5. Fatou Samba Ndiaye, mtu mashuhuri katika tiba nchini Senegal
Chanzo cha picha, Getty Images
Akiwa mhimili muhimu katika utafiti na uongozi wa kitabibu wa wanawake barani Afrika, Profesa Fatou Samba Ndiaye ni mtaalamu mashuhuri wa damu (hematolojia) kutoka Senegal, aliyebobea katika saratani za damu na tiba ya seli.
Akiwa mkuu wa idara ya hematolojia na kitengo cha upandikizaji wa uboho katika Hospitali ya Dalal Jamm huko Guédiawaye, Dakar, ni miongoni mwa waanzilishi wa upandikizaji wa uboho nchini Senegal.
Amechukua nafasi muhimu katika kuandaa, kuimarisha na kuendeleza idara hiyo.
Kwa mujibu wake, kuwa mwanamke hakukumzuia kupitia miaka mingi ya masomo iliyohitajika ili kuwa mtaalamu wa ngazi ya juu katika taaluma hii. Alipambana kwa juhudi kubwa hadi kufikia uongozi wa idara hiyo nchini Senegal.
Akiwa Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake wa Senegal, Bi. Ndiaye amechapisha tafiti nyingi katika majarida ya kimataifa, na pia ni mkaguzi wa kwanza katika Kitivo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop cha Dakar.
Mnamo Januari 2022, Fatou Samba Ndiaye alitunukiwa tuzo ya Knight of the National Order of the Lion, kabla ya kupandishwa hadhi kuwa Afisa wa National Order of the Lion mwaka 2024.
Profesa Fatou Samba Ndiaye ni kielelezo muhimu katika tiba ya Senegal, akiiacha alama katika taaluma yake kupitia utaalamu wa kisayansi, kujitolea kwa jamii na uongozi wa wanawake.
6. Mpumi Madisa, kiongozi aliyejidhihirisha
Chanzo cha picha, Bidvest Group/Facebook
Nompumelelo Thembekile Madisa, anayejulikana kama Mpumi Madisa, ni mfanyabiashara kutoka Afrika Kusini, na mwanamke wa kwanza kuwa Mkurugenzi Mtendaji (CEO) wa kundi shirikisho la viwanda la Bidvest, ambalo linaajiri watu 137,000.
Pia ndiye mwanamke mweusi wa kwanza kuwa CEO wa makampuni yaliyo kwenye orodha ya 40 bora ya Johannesburg Stock Exchange (JSE), soko kubwa zaidi la hisa barani Afrika.
“Kuteuliwa kwa Mpumi Madisa kuwa CEO wa kampuni kubwa katika uchumi wetu ni mafanikio makubwa binafsi, na pia ni hatua zaidi kuelekea usawa wa kijinsia katika biashara.
Hivyo basi, uteuzi wa Bi. Mpumi Madisa ni tukio la kusherehekea na pia kuimarisha ahadi ya kuharakisha mabadiliko na maendeleo katika ngazi za juu za uchumi wetu,” alisema Rais Cyril Ramaphosa.
Akiwa na shahada ya uzamili (master’s) katika fedha na uwekezaji, yeye ni mjumbe wa bodi ya makampuni 16 ya Bidvest, bodi ya wakurugenzi ya Adcock Ingram, na Business Leadership South Africa.
Mpumi Madisa ni miongoni mwa wanawake 50 wenye ushawishi mkubwa barani Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes.
7. Judith Suminwa Tuluka, waziri mkuu mwanamke
Chanzo cha picha, Getty Images
Amekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya demokrasia ya Congo (DRC) tangu mwaka 2024, nafasi isiyokuwa ya kawaida kwa mwanamke katika nchi hii.
Judith Suminwa Tuluka ameonyesha utaalamu wake katika uchumi wa nchi yake na imechukua nafasi muhimu kwenye uongozi wa serikali, jambo ambalo limeimarisha uaminifu wa uongozi wake.
“Ninafahamu uzito mkubwa wa jukumu langu, na nimeeleza kwa kiongozi wa nchi kuwa anaweza kutegemea uaminifu wangu kumsaidia kuongoza kwa mafanikio maendeleo ya nchi yetu.
Alipokuwa akiapishwa aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya nchi na maendeleo yake.
“Jukumu ni kubwa, changamoto ni nyingi,” alisema kwa vyombo vya habari masaa kadhaa baada ya uteuzi wake mnamo Aprili 4, 2024.
Akiwa na Shahada ya Uzamili katika Uchumi (Applied Economics), aliyebobea katika usimamizi wa fedha kutoka Kitivo cha Uchumi, Mons, Ubelgiji, Judith Tuluka Suminwa pia alipata shahada ya uhasibu kutoka Shule ya Elimu Endelevu na Mafunzo (EPFC) huko Brussels.
Mwanamke huyu, ambaye yuko miongoni mwa wanawake 50 wenye ushawishi mkubwa barani Afrika, alianza kazi yake kwa mwaka mmoja Citibank, kisha alifanya kazi kwa muda mrefu katika mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na UNDP, kabla ya kurudi DRC na kujiunga na taaisis za umma hasa Wizara ya bajeti kama mshauri wa Kitengo cha mabadiliko ya hali ya biashara.
Judith Tuluka Suminwa alishikilia wadhifa wa Waziri wa nchi, Waziri wa Mipango, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.
Ngozi Okonjo-Iweala, taswira ya sekta ya fedha nchini Nigeria
Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamke kutoka Nigeria, Ngozi Okonjo-Iweala, ni kielelezo cha juu katika diplomasia ya kifedha ya nchi yake.
Akijulikana duniani kote kwa kazi yake iliyojizatiti kwa uchumi wa dunia, anafurahia kutambulika kimataifa.
Akiwa Waziri wa Fedha wa Nigeria kutoka mwaka 2003 hadi 2006 na 2011 hadi 2015, alikua mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huu na kusaidia kupunguza ufisadi na deni la umma nchini mwake.
Bi. Okonjo-Iweala alifanya kazi kwa miaka 25 katika Benki ya Dunia (World Bank), ambapo alipanda hadi kufikia wadhifa wa pili kwa ukubwa kama Mkurugenzi Mtendaji.
Alijumuishwa kwenye orodha ya 50 bora ya viongozi wakubwa zaidi duniani katika jarida la Fortune mwaka 2015, na mnamo 2020 alitambulika kama nyota wa Afrika na jarida la Forbes, ambalo tayari liliorodhesha miongoni mwa Wanawake 100 Wenye ushawishi zaidi duniani kwa miaka minne mfululizo.
Mwaka huu, tena anaonekana katika orodha ya Wanawake 50 bora barani Afrika.
Bi. Okonjo-Iweala ana shahada ya kwanza katika uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Harvard na shahada ya udaktari (PhD) kutoka Massachusetts Institute of Technology (MIT).