
Unguja. Watafiti na wasaidizi wa kisheria wametakiwa kuhakikisha wanakusanya taarifa sahihi ili kupata matokeo halisi yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa haki za binadamu nchini.
Hayo yameelezwa leo Alhamis Desemba 18, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Zanzibar (ZLSC), Felista Mauya wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watafiti watakaoshiriki katika utafiti wa hali ya msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki za binadamu visiwani Zanzibar, utakaofanyika mwezi huu.
Felista amesema lengo la utafiti huo ni kufanya tathmini na kupata taarifa za awali kuhusu viashiria vitakavyotumika kupima mafanikio ya utekelezaji wa haki za binadamu, hususan haki za kiraia na kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Amesema utafiti huo utaangalia namna haki hizo zinavyolindwa kisheria na vyombo mbalimbali visiwani Zanzibar, ili kubaini changamoto zilizopo na maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi.
“Taarifa zitakazokusanywa zitaiwezesha ZLSC kupata uhalisia wa upatikanaji wa haki za binadamu na hivyo kuboresha mikakati ya utekelezaji kulingana na hali halisi katika kila wilaya za Zanzibar,” amesema.
Hata hivyo, amewasisitiza watafiti hao kuzingatia ukweli na uadilifu wakati wa ukusanyaji wa taarifa hizo, ili kuepuka zile zinazopotosha umma na kuharibu taswira ya taasisi na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Castor Kalemera, mtafiti kiongozi wa haki za binadamu, amewaomba wananchi watakaofikiwa na utafiti huo kutoa taarifa za ukweli kwa masilahi ya jamii na taifa kwa ujumla.
Amesema, utafiti huo utahusisha watu 608 kutoka wilaya 11 za Zanzibar, wakiwemo wananchi wa makundi mbalimbali, watendaji wa Serikali, taasisi binafsi na asasi za kiraia.
Kalemera amesema utafiti huo utafanyika kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwamo ya mahojiano ya ana kwa ana na majadiliano ya vikundi, huku matumizi ya teknolojia yakizingatiwa kupata takwimu sahihi.
Akizungumzia utafiti wa awali uliofanywa na ZLSC mwaka 2024, amesema uliwahusisha watu 300, matokeo yalionyesha kuwa asilimia 66 ya waliohojiwa waliripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wakati katika mamlaka husika, asilimia 20 hawakuripoti na asilimia 14 hawakuwa na uhakika.
Pia, amesema asilimia 77 waliamini kuwa viongozi wao wanaheshimu na kulinda haki za binadamu, asilimia 14 walidai hawafanyi hivyo huku asilimia tisa wakisema hawakuwa na uhakika.
“Asilimia 72 walihisi wanafurahia uhuru wa kutoa maoni na kukusanyika, asilimia 25 hawakufurahia haki hiyo na asilimia nne hawakuwa na uhakika,” amesema Kalemela.
Naye Mshiriki wa mafunzo hayo, Halima AbdulKadir Mohamed amesema katika utafiti uliopita walikumbana na changamoto ya ushiriki mdogo kutoka kwa baadhi ya wananchi.
Hivyo, amewaomba masheha kuwahamasisha wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati.