RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar ina fursa nyingi za kiuchumi, hususan katika sekta ya Uchumi wa Buluu na uwekezaji, hivyo amewahimiza viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutumia majukwaa ya kimataifa kuitangaza Zanzibar ili inufaike zaidi kiuchumi.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 19 Desemba 2025, alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Mambo ya Nje, Mhe. Dk. Ngwaru Jumanne Maghembe, pamoja na Naibu Waziri anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya, waliofika Ikulu Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa sekta ya mambo ya nje ni ya Muungano, hivyo ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili Zanzibar iweze kunufaika kikamilifu na utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi, fursa za kimataifa pamoja na kutangazwa kwa vivutio na fursa za uwekezaji zilizopo visiwani humo.

Aidha, amesisitiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuweka mkazo maalum kwa Zanzibar katika ushiriki wa jumuiya za kimataifa, ili kuhakikisha inanufaika zaidi na fursa za maendeleo na kiuchumi zinazopatikana kupitia ushiriki huo.

Rais Dk. Mwinyi amebainisha umuhimu wa upatikanaji wa misaada na mikopo ya kimataifa, na kuwataka Naibu Mawaziri hao kuweka mikakati mahsusi itakayohakikisha Zanzibar inazingatiwa ipasavyo na kunufaika kwa wakati na rasilimali hizo.

Vilevile, ameonesha kuridhishwa na ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kuwahakikishia viongozi hao kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kwa lengo la kuwatumikia wananchi wa Tanzania kwa ufanisi, ikiwemo Zanzibar.

Kwa upande wao, Naibu Mawaziri hao wamempongeza Rais Dk. Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata katika Uchaguzi Mkuu, pamoja na juhudi anazoendelea kuzifanya katika kuiletea maendeleo Zanzibar. Wamesifu mageuzi makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na miundombinu ya barabara, na kuahidi kutekeleza kwa vitendo maelekezo na ushauri uliotolewa na Rais Dk. Mwinyi. SOMA: Serikali yajivunia tija diplomasia ya uchumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *