gg

Chanzo cha picha, EPA

Umoja wa Ulaya umebadilisha mkakati wa kusaidia Ukraine kwa kuamua kukopa fedha kwa pamoja badala ya kutumia mali za Urusi zilizozuiwa kutumika.

Viongozi wa EU walikubaliana Ijumaa kutoa msaada wa euro bilioni 90 kwa Ukraine katika kipindi cha mwaka 2026 hadi 2027 ili kusaidia ulinzi wake dhidi ya Urusi.

Fedha hizo zitapatikana kupitia mikopo kutoka masoko ya mitaji, ikidhaminiwa na bajeti ya Umoja wa Ulaya.

Makubaliano hayo hayatawalazimisha Hungary, Slovakia na Jamhuri ya Czech kushiriki katika ufadhili huo, kwani nchi hizo hazikuwa tayari kuchangia msaada kwa Ukraine.

Hata hivyo, EU itaendelea kujadili mpango wa mkopo utakaotegemea mali za benki kuu ya Urusi zilizozuiwa kutumika.

Mkopo huo utalipwa na Ukraine pale itakapopokea fidia ya vita kutoka Urusi.

Hadi wakati huo, mali za Urusi zitaendelea kuzuiwa, na EU itabaki na haki ya kuzitumia kulipa mkopo endapo italazimika.

Wanadiplomasia wamesema uamuzi huu unahakikisha Ukraine inapata ufadhili wa uhakika kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Awali, viongozi wa EU walijaribu kutumia mali za Urusi zilizozuiwa kutumika moja kwa moja, lakini mpango huo ulionekana kuwa mgumu kiteknolojia na kisiasa.

Changamoto kubwa ilikuwa ni kuilinda Ubelgiji, ambako mali nyingi za Urusi barani Ulaya zimehifadhiwa, dhidi ya hatari za kifedha na kisheria zinazoweza kutokea iwapo Urusi ingerudisha mashambulizi ya kiuchumi au kisheria.

Kwa hatua hii, EU inalenga kuhakikisha msaada kwa Ukraine unaendelea bila kucheleweshwa, huku ikiepuka migogoro ya kisheria na kisiasa ndani ya umoja huo.

Haya yanajiri baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kusema Urusi itatwaa maeneo zaidi nchini Ukraine kwa kutumia nguvu iwapo Kyiv na wanasiasa wa Ulaya aliowaita “nguruwe” hawatakubali mapendekezo ya Marekani kuhusu makubaliano ya amani.

Akizungumza katika mkutano wa kila mwaka wa masuala ya ulinzi ya Urusi, Putin alisema nchi yake inapiga hatua katika pande zote za vita na akasisitiza kuwa Urusi itatimiza malengo yake ama kwa njia ya diplomasia au kwa nguvu, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unaendesha mazungumzo tofauti na Moscow na Kyiv, pamoja na viongozi wa Ulaya, kuhusu mapendekezo ya kumaliza vita nchini Ukraine.

Hata hivyo, hadi sasa hakujapatikana makubaliano.

Kyiv na washirika wake wa Ulaya wana wasiwasi kuhusu madai ya Urusi yanayosisitiza kuyatwaa maeneo ya Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *