Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, MariamMjahid
- Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
-
Muda wa kusoma: Dakika 5
Wakati milio ya kengele za Krismasi inaanza kusikika na maduka yakijaa kwa harakati za ununuzi, furaha ya msimu huu inaweza haraka kubadilika kuwa karaha kwa baadhi ya watu hasa pale unaponaswa kwenye mtego wa walaghai wa mitandaoni.
Krismasi ni kipindi cha upendo, zawadi na sherehe. Wengi hufanya maandalizi makubwa, wakinunua vyakula, mavazi mapya, na zawadi kwa wapendwa wao.
Lakini kipindi hiki pia ni wakati unaopendwa zaidi na wahalifu wa mtandaoni, ambao hutumia udhaifu wa wateja na msisimko wa sherehe kufanya uhalifu wao kwa ustadi mkubwa.
Zaidi ya simu 17,300 zimezimwa kutokana na kutumika katika vitendo vya utapeli na uhalifu mtandaoni katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita nchini Tanzania.
Dkt. Jabir Bakari, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, alithibitisha jambo hilo kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, alipowasilisha ripoti ya utendaji wa sekta, akibainisha kuwa viashiria vya matukio ya utapeli kwa simu vinaendelea kupungua.
Vitendo hivyo na hatua zilizochukuliwa vilipungua kutoka kwenye simukadi 20,939 zilizoorodheshwa kama hatari kati ya Oktoba hadi Desemba 2023, hadi laini 17,318 zilizozimwa kati ya Januari hadi Machi 2024, ikionyesha kupungua kwa asilimia 15% Tanzania.
Hata hivyo, kupungua huko hakumaanishi kuwa wahalifu wameenda likizo bado wizi wa mitandaoni umeendelea kuwapatia hasara wanunuzi.
Chanzo cha picha, Getty Images
Walaghai wanavyotumia furaha ya sikukuu kama fursa
Katika miaka ya karibuni, kuongezeka kwa biashara za kidijitali kumebadilisha kabisa namna Watanzania na Wakenya wanavyonunua bidhaa.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka SlashNext, uhalifu wa mtandaoni ulimwenguni ulipanda kwa asilimia 703 mwaka 2024 pekee. Hali hii inaonyesha wazi jinsi walaghai wanavyozidi kuwa wabunifu na kutumia teknolojia kisasa kuwalaghai watumiaji wasio na tahadhari.
Kulingana na Better Business Bureau, shirika lisilo la faida ambalo linashughulikia malalamiko ya watumiaji, tovuti bandia ni mojawapo ya ulaghai mkuu ulioripotiwa.
Haya yalisababisha hasara ya mauzo ya takriban dola milioni 380 nchini Marekani mwaka wa 2022. Kwa hakika, hasara hiyo huenda ikawa kubwa zaidi ikizingatiwa kwamba visa vingi haviripotiwi.
Mitego ya kisasa inavyotumika
Chanzo cha picha, Getty Images
Walaghai wa mtandaoni hawana mipaka wanaweza kuwa popote, lakini hupendelea watu wanaonunua bidhaa mtandaoni.
”it’s Black Friday” ni kauli husheheni kwa maduka mengi nchini Kenya, huku watu wakifurika kwa mitandao kununua bidhaa kwa bei ya kipunguzo.
Katika hali hiyo hujipata wameweka maelezo yao ya siri kama vile nambari za simu ambazo pia hutumiwa na wahalifu kuwaibia.
Wengi wao hutumia mbinu zifuatazo:
1.Tovuti Bandia: Wanaiga muonekano wa tovuti maarufu za biashara, kisha kuweka bidhaa kwa bei ya chini kupita kiasi ili kuvutia wanunuzi.
2.Ujumbe wa Kivutio: Hutuma SMS au barua pepe zenye ujumbe kama “Umeshinda zawadi ya Krismasi!” au “Punguzo maalumu hadi 80% leo pekee.” Ujumbe huo huambatana na kiunganishi (link) kinachowaongoza watumiaji kwenye tovuti ya kitapeli.
3.Simu za Kudanganya: Wapo wanaopiga simu wakijifanya wahudumu wa benki au kampuni ya simu, wakikuomba “kuthibitisha” taarifa zako za akaunti. Mara unapotoa taarifa hizo, pesa zako hutoweka kimya kimya.
4.Fomu za Usajili Bandia: Hutoa fomu ndefu zinazohitaji taarifa binafsi, ikiwemo majina kamili, namba ya kitambulisho na taarifa za kadi ya benki, kisha huzitumia kuiba au kufanya miamala isiyo halali.
Athari zinavyowaathiri waathiriwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa baadhi ya waathiriwa, uhalifu huu ni zaidi ya kupoteza pesa.
Ni kuvunjika kwa imani. Habiba Mussa, mkazi wa Nairobi, anasimulia jinsi alivyoibiwa zaidi ya shilingi elfu sita baada ya kufanya ununuzi mtandaoni.
“Niliona tangazo la mavazi ya Krismasi kwenye Tiktok, bei ilikuwa nzuri sana. Nililipa kupitia simu, lakini bidhaa haikuwahi kufika. Niliwasiliana nao, wakasema ‘mzigo upo njiani’. Baada ya siku tatu, namba yao haikupatikana tena,” anasema Habiba kwa masikitiko.
Tukio kama hili limekuwa la kawaida. Wengi hukosa kujua namna ya kuchukua hatua, na walaghai hupotea bila kuchukuliwa sheria.
Jinsi ya kujilinda dhidi ya walaghai
Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini utafiti wetu uligundua kuwa kuna jambo moja rahisi unaweza kufanya ili kupunguza kwa kiasi kikubwa nafasi zako za kupoteza pesa kwa ulaghai wa mtandao: punguza kasi.
Kwa hakika, miongoni mwa mbinu nyingi ambazo walaghai hutumia, kujenga hisia ya uharaka au hitaji la kuchukua hatua au kujibu haraka pengine ndiyo yenye kudhuru zaidi.
Kama ilivyo kwa mauzo mengi halali, kutenda haraka kunapunguza uwezo wako wa kufikiri kwa makini, kutathmini taarifa na kutofanya uamuzi wa tahadhari.
Wataalamu wa teknolojia wanasema suluhisho lengine ni ufahamu. Ili usiwe miongoni mwa waathiriwa, zingatia hatua hizi muhimu:
Nunua kupitia tovuti salama – Kabla ya kulipia bidhaa, hakikisha tovuti inaanza na https:// badala ya http://. na ina alama ya kufuli karibu na anwani yake.
Tumia nenosiri imara – Unda nywila tofauti kwa kila akaunti na ibadilishe mara kwa mara. Epuka kutumia majina au tarehe rahisi kubashiriwa.
Soma maoni ya wateja – Tathmini na ushuhuda wa wateja wengine ni kipimo kizuri cha uhalali wa tovuti. Ikiwa hakuna maoni, kuwa makini.
Tumia njia salama za malipo – Kadi za benki au mifumo rasmi kama PayPal hutoa ulinzi zaidi kuliko kutuma pesa taslim au kwa akaunti binafsi.
Weka programu za ulinzi – Simu na kompyuta ziwe na programu za kupambana na virusi zilizosasishwa mara kwa mara.
Epuka ofa zisizo za kweli – Ofa inayovutia kupita kiasi mara nyingi ni mtego. Ukiona punguzo lisilo la kawaida, chukua muda kuchunguza.
Serikali na taasisi zina nafasi kubwa
Wataalamu wanashauri pia serikali kuimarisha ufuatiliaji wa makosa ya kimtandao.
Mnamo mwaka 2024, mamlaka hiyo ilizindua kampeni ya “Jihadhari Mtandaoni” yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu usalama wa taarifa binafsi.
Hata hivyo, bado changamoto kubwa ipo katika elimu ya watumiaji, hasa vijana na wazee ambao mara nyingi huamini kila wanachoona mtandaoni.
Kwa kweli, labda ushauri bora zaidi unaweza kuuchukua ni: usiharakishe kufanya mambo mtandaoni.