Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani kwa maneno makali uhalifu na kitendo kiovu kilichofanywa na Mmarekani cha kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu, ikielezea tukio hilo kuwa la kichochezi linalotoa harufu mbaya ya chuki, na shambulio la wazi dhidi ya matakatifu zaidi ya Waislamu na maadili ya kidini na ya kibinadamu yanayowakilishwa na dini zote za mbinguni.
Taarifa iliyotolewa jioni ya jana na Hizbullah imesema: “Utamaduni wa ubaguzi wa rangi na matamshi ya chuki yanayochochewa na mirengo ya kisiasa na vyombo vya habari vya Magharibi ndiyo sababu kuu ya uhalifu huu.” Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Serikali zilizofuatana za Marekani na ushawishi wa Wazayuni vimekuwa “vikifanya uchochezi kwa miongo kadhaa kupotosha taswira ya Uislamu ili kuhudumia miradi ya kuibua fitina, ya kikoloni na uharibifu.”
Harakati ya Hizbullah imesema, kukataa utawala wa Marekani kuchukua hatua dhidi ya wahusika wa uhalifu huu, kwa kisingizio cha “uhuru wa uongo eti wa maoni na kujieleza,” ni uthibitisho kwamba serikali hiyo inahalalisha kikamilifu vitendo vya kichochezi.
Taarifa hiyo imesema: “Uhalifu huu si kitendo cha mtu binafsi, bali wahusika wake ni wanasesere na vibaraka wanaotumiwa na ubeberu wa kimataifa unaotaka kudhoofisha dini ya Uislamu kama mfumo wa maadili unaokabiliana na utovu wa maadili na uhalifu unaoendelezwa duniani.”
Hizbullah imetoa wito kwa Umma wa Kiarabu na Kiislamu katika matabaka yake yote, viongozi, mamlaka za kidini na kitamaduni, pamoja na wafuasi wa dini zote za mbinguni, kushiriki katika “kampeni pana zaidi ya kulaani kitendo hiki kibaya cha kihalifu.”