RAUNDI ya 11 ya Ligi ya Championship inaendelea tena wikiendi hii, huku macho na masikio ya wapenzi wa soka yakielekezwa katika mechi ya kesho Jumapili kati ya Geita Gold na Kagera Sugar, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.
Mechi hii inasubiriwa kwa hamu kutokana na rekodi za makocha wa timu hizo msimu huu na Geita Gold inayofundishwa na Zubery Katwila na Kagera Sugar inayonolewa na Juma Kaseja zimekuwa na mwenendo mzuri, jambo linalovutia zaidi.
Geita inaongoza Ligi ya Championship ikiwa na pointi 28, sawa na Kagera Sugar baada ya kikosi hicho kushinda mechi tisa na kutoka sare mmoja, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 21 na ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu.
Kwa upande wa Kagera Sugar, inashika nafasi ya pili na pointi 28, kama ilivyo za Geita, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tisa pia na kutoka sare mmoja, ikifunga mabao 20 na kuruhusu matatu, hivyo, kutofautiana kileleni kwa bao moja tu.
Timu zote zinakutana zikiwa na morali nzuri baada ya kushinda mechi za mwisho zikiwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na Geita iliichapa TMA mabao 2-1, huku Kagera Sugar ikiondoka na ushindi wa 2-0, dhidi ya Mbuni.
Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.
Timu hiyo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Kwa upande wa Kagera iliyodumu Ligi Kuu kwa miaka 20 tangu iliposhiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 na kwenye mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu huko mjini Geita, hakuna aliyeibuka kidedea, baada ya kutoka suluhu (0-0), Februari 28, 2024.
Mechi hiyo ilikuwa ya raundi ya pili, baada ya ile ya kwanza iliyopigwa Septemba 16, 2023, kwenye Uwanja wa Kaitaba na kumaliziwa Septemba 17, 2023, baada ya taa kuzima na kuisha Kagera ikishinda bao 1-0, la beki, Mganda Dissan Galiwango.
Iko hivi. Mechi hiyo awali ilipangwa kuchezwa Septemba 16, 2023, ila ilichezwa kwa dakika 39, baada ya taa za Uwanja wa Kaitaba kuzima hivyo, kuendelea tena Septemba 17, 2023, ndipo wenyeji walipopata bao hilo la beki huyo dakika ya 90+4.
Kocha wa Geita, Zubery Katwila amesema licha ya presha ya mechi hiyo kutokana na nafasi za kila timu, ila wamekamilisha maandalizi yote muhimu, ikiwemo kuwasoma wapinzani na jinsi ya kukabiliana nao kwa nidhamu ili kupata pointi tatu.
Kwa upande wa Kocha wa Kagera, Juma Kaseja amesema mechi hii siyo ya kuamua hatima ya timu hizo katika nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara kwa sababu bado ni mapema, japo ukubwa wake unaweza ukatoa taswira kutokana na mwenendo ulivyo hadi sasa.
Mechi nyingine za kesho Jumapili, Stand United iliyoichapa Barberian bao 1-0, itaikaribisha Gunners iliyochapwa 1-0 na Transit Camp, huku Bigman iliyoifunga Hausung 1-0, ikiikaribisha Mbeya Kwanza iliyoichapa B19 zamani Tanesco mabao 5-0.
B19 yenye kumbukumbu mbaya baada ya kufungwa mabao 5-0, dhidi ya Mbeya Kwanza, itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro kucheza na Hausung FC, huku mechi ya mwisho ni kati ya maafande wa Transit Camp watakaoikaribisha kikosi cha Barberian.
Leo Jumamosi zitapigwa mechi tatu na kutakuwa na ‘Arusha Monduli Derby’, kati ya TMA iliyochapwa mabao 2-1 na Geita Gold, itakayowakaribisha Mbuni iliyofungwa 2-0, dhidi ya Kagera Sugar, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Maafande wa Polisi Tanzania itakuwa kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi kucheza na African Sports, huku mechi ya mwisho leo Jumamosi itapigwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea, kati ya wenyeji, Songea United dhidi ya KenGold.