Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imelaani vikwazo vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya majaji wawili wa korti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Siku ya Alkhamisi, ICC ilielezea vitendo vya Washington dhidi ya Jaji Gocha Lordkipanidze wa Georgia na Jaji Erdenebalsuren Damdin wa Mongolia kama “shambulio baya” dhidi ya uhuru wa taasisi ya mahakama isiyo na upendeleo.

“Vikwazo hivi ni hujuma mbaya dhidi ya uhuru wa taasisi ya mahakama isiyo na upendeleo ambayo inafanya kazi kwa mujibu wa mamlaka iliyotolewa na Mataifa Wanachama kutoka maeneo mbalimbali,” ICC ilmesema katika taarifa.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu vikwazo vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya majaji wawili wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), akisisitiza jukumu la mahakama hiyo katika kuhakikisha haki kimataifa.

Jana Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio alitangaza vikwazo dhidi ya majaji wa ICC, Gocha Lordkipanidze wa Georgia na Erdenebalsuren Damdin wa Mongolia, akiwatuhumu kwa eti “kuhusika moja kwa moja” katika “kulenga Israel kinyume cha sheria.”

Hapo awali, Marekani ilikuwa imewaadhibu maafisa wa mahakama ICC kwa kuidhinisha hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa Vita, Yoav Gallant kwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza huko Palestina. Katika taarifa yake, ICC ilionya kwamba kuwatishia majaji kwa kuheshimu sheria kunahatarisha mfumo mzima wa kisheria wa kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *