Jenerali Mkuu wa Sudan, Abdel-Fattah al Burhan, amekutana na Rais wa Misri, Abdel-Fattah el-Sissi mjini Cairo huku kukiwa na shinikizo linalozidi kuongezeka la kuhimiza kutatuliwa mgogoro wa vita nchini Sudan haraka iwezekanavyo.

Mazungumzo baina ya Jenerali al Burhan na Jenerali elSissi yamekuja baada ya mkuu huyo wa jeshi la SAF la Sudan kufanya mazungumzo na maafisa wa Saudi Arabia mjini Riyadh mapema wiki hii. Mjumbe wa Marekani, Massad Boulos pia alikuweko Riyadh wakati huo kwa ajili ya kufanya mazungumzo na maafisa wa Saudi Arabia. Hakuna taarifa zozote rasmi zilizotolewa kuhusu iwapo Jenerali al Burhan alikutana na afisa huyo wa Marekani huko Riyadh au la.

Katika taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo ya Jenerali al Burhan na Jenerali el Sisi, pande mbili zimethibitisha kwamba Cairo inaiunga mkono serikali ya al Burhan lakini pia kuna “mistari nyekundu” ambayo Misri inasema haipaswi kuvukwa.

Taarifa ya Ikulu ya Misri imesema kwamba Cairo inatilia mkazo “haki yake kamili ya kuchukua hatua zote muhimu na zinazokubaliwa na sheria za kimataifa na Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi kati ya nchi hizo mbili ndugu ili kuhakikisha kwamba mistari hiyo nyekundu haivukwi.”

Sudan ilitumbukia katika machafuko mwezi Aprili 2023 kutokana na uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF. Vita hivyo, ambavyo hivi sasa viko katika mwaka wake wa tatu, vimeshaua zaidi ya watu 40,000. Takwimu hizo zimetolewa na Umoja wa Mataifa, lakini makundi ya misaada yanasema kuwa hiyo ni idadi ndogo sana kwani idadi halisi inaweza kuwa kubwa mara nyingi zaidi kuliko hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *