Chanzo cha picha, AFP
-
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
-
Muda wa kusoma: Dakika 6
Wafanyakazi nchini Kenya watalazimika kulipa hadi Sh2,160 zaidi kwa mwezi kwenye Hazina ya kitaifa ya Hifadhi ya Jamii {NSSF}kuanzia Februari 2026, kutokana na ongezeko la kiwango cha michango ya lazima ya pensheni. Hii itazidisha mzigo wa kifedha kwa familia huku gharama za maisha zikiongezeka.
Mjadala wa makato ya serikali ili kugharamia uchumi wa nchi ulianza kujipenyeza tangu wakenya kulazimika kulipa asilimia tatu ya mshahara wao ili kuhudumia hazina mpya ya Maendeleo ya Makaazi.
Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa malipo hayo sio kodi bali ni akiba ingawa makato hayo yatalindwa na sheria na kutolewa kwa mishahara ya wafanyakazi.
Na makato hayajaishia hapo, mshahara wa walioajiriwa pia umepungua zaidi kufuatia nyongeza ya ada kwa mfuko wa huduma ya afya ya jamii yaani SHIF.
Watakaotozwa zaidi
Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na mfumo mpya, wafanyakazi wanaopata mshahara wa zaidi ya Sh100,000 kwa mwezi watalipa Sh6,480 kila mwezi, kutoka kiwango cha sasa cha Sh4,320. Wale wanaopata chini ya Sh100,000 michango yao itapanda hadi Sh6,000 kutoka Sh4,320.
Hata hivyo, wafanyakazi wenye mapato ya chini ya Sh50,000 kwa mwezi hawataathirika na ongezeko hilo, na wataendelea kulipa kati ya Sh1,500 na Sh2,100 kulingana na kipato chao.
Ongezeko hili linafuata mageuzi ya hivi karibuni kwenye NSSF, ambayo yamegawanya mchango wa pensheni wa lazima wa asilimia 12 kwa usawa kati ya mwajiri na mfanyakazi.
Mwaka jana, NSSF pia iliongeza kiwango cha juu cha michango, ambapo safu ya kwanza iliongezeka hadi Sh960 kwa mwezi, na safu ya pili kwa wale wanaopata mshahara wa zaidi ya Sh70,000 ilipanda hadi Sh8,400.
Ongezeko la hivi karibuni linatarajiwa kuongeza shinikizo kwa wafanyakazi ambao tayari wanakabiliana na kupungua kwa uwezo wa kununua, kutokana na mfumuko wa bei, kodi kubwa na makato mengine ya lazima.
Mageuzi ya NSSF yanalenga kuongeza akiba za kustaafu na kuboresha usalama wa pensheni kwa muda mrefu, lakini wakosoaji wanasema kuwa muda wa ongezeko hili unaweza kuongeza matatizo ya kifedha kwa wafanyakazi wasio na kandarasi ya kudumu.
Utekelezwaji wa hazina ya NSSF
Chanzo cha picha, Getty Images
Huu ni mwaka wa nne wa utekelezaji wa ongezeko la michango ya lazima ya NSSF.
Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ya mwaka 2013 imepitia marekebisho kadhaa katika miaka ya karibuni.
Mabadiliko hayo yamehusisha kuongezwa kwa viwango vya michango, kupanuliwa kwa wigo wa wachangiaji ili kuwajumuisha wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi, pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa ngazi mbili za michango.
Baada ya Sheria hiyo kuanza kutekelezwa, Chama cha Wakulima wa Chai Kenya (KTGA) pamoja na wadau wengine waliwasilisha kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa NSSF, wakipinga baadhi ya vipengele vya Sheria hiyo.
Kesi hiyo ilikamilika tarehe 21 Februari 2024, pale Mahakama ya Juu ilipotoa uamuzi katika kesi ya Kenya Tea Growers Association na wengine watatu dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa NSSF na wengine. Mahakama ilithibitisha uamuzi wa awali wa Mahakama ya Rufaa, ambao ulitangaza kuwa Sheria ya NSSF ni halali kisheria.
Mahakama ya Rufaa ilikuwa tayari, tarehe 3 Februari 2023, imethibitisha uhalali wa Sheria hiyo, na hivyo utekelezaji wa michango ukaanza rasmi Februari 2023 na kuendelea.
Athari ya nyongeza ya ada
Nyongeza hii ya ada ya pensheni itaathiri ununuaji wa bidhaa kwa kuwa wafanyakazi watabaki na fedha kidogo kugharamia maisha ambayo mfumko wa bei za bidhaa za kimsingi unashuhudiwa barani Afrika.
Wataalam wa uchumi wanaeleza kuwa huenda hakuna matumaini ya afueni kupatikana hivi karibuni hasa katika sekta ya biashara ambayo imekuwa ikisuasua tangu janga la Covid-19.
Kwa upande mzuri, usalama wa kifedha wa mfanyakazi utaimarishwa kwa muda mrefu kama viwango vyao vya akiba vinaongezeka katika NSSF.
Kwa upande wa waajiri, mabadiliko haya yatasababisha kuongezeka kwa gharama za kuajiri na kumudu wafanyakazi, pamoja na kuongezeka kwa majukumu ya kufuata sheria, hasa ikizingatiwa makato mengine ya lazima kama Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii, tozo ya Makazi Nafuu na viwango vipya vya PAYE vilivyotekelezwa katika miaka ya karibuni.
Mkusanyiko wa mabadiliko haya katika makato ya lazima utaathiri mipango ya rasilimali watu na gharama za uendeshaji, na kuwalazimu kupitia upya mikakati yao ya mishahara na mafao.
Kwa upande chanya, kutambuliwa kwa tozo ya Makazi Nafuu na michango ya Bima ya Afya ya Jamii kama makato yanayoruhusiwa kunapunguza kipato kinachotozwa kodi, na hivyo kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi. Hata hivyo, ongezeko la michango ya NSSF litaendelea kupunguza mshahara halisi na kipato kinachobaki kwa matumizi binafsi.
Kwa muda mrefu, usalama wa kifedha wa wafanyakazi utaimarika kutokana na kuongezeka kwa akiba zao ndani ya NSSF.
Kwa nini Rais wa Kenya anataka wananchi waipende mamlaka ya kodi
Chanzo cha picha, Reuters
Wakenya wanaanza kuthibitisha msemo wa zamani kwamba mambo mawili pekee yasiyoepukika maishani ni kifo na kodi.
Hali hii inatokana na juhudi za Rais William Ruto kuwashawishi wananchi wake kuwa wanapaswa kulipa kodi zaidi, akisisitiza kuwa kwa hali ilivyo sasa, bado hawatozwi kodi ya kutosha.
Hivi karibuni, Rais Ruto alisema kuwa Wakenya “wamelelewa kuamini kuwa wanalipa kodi nyingi kuliko nchi nyingine,” ilhali kwa mujibu wake, mzigo wa jumla wa kodi nchini Kenya bado ni mdogo ukilinganishwa na baadhi ya nchi barani Afrika na kwingineko duniani.
“Lazima tuongeze makusanyo ya kodi,” alisema, huku akikiri kuwa hatua hiyo “haitakuwa rahisi”.
Tangu achaguliwe kuwa Rais mwezi Agosti 2022, serikali ya Ruto imeongeza aina mbalimbali za kodi na pia kuanzisha kodi mpya kama tuliyoianisha mwanzo wa makala yetu.
Ujumbe wa Rais Ruto ni kwamba ikiwa wananchi wanataka huduma bora za umma na kupunguza deni la taifa, basi hawana budi kuchangia zaidi kupitia kodi.
Hata hivyo, Wakenya wengi hawaridhiki.
Uanzishwaji wa baadhi ya kodi hizo mpya, sambamba na kupanda kwa gharama za maisha, ulisababisha maandamano makubwa ya mitaani mwaka 2023 na kuvuka hadi 2024, ambayo yalipelekea vifo vya vijana wengi waliokuwa wanataka mabadiliko.
Kwa sasa, mazungumzo ya kila siku miongoni mwa raia wa Kenya mara nyingi hutawaliwa na malalamiko kuhusu mzigo wa kodi, huku kauli za Rais zikiongeza hasira kwa Wakenya ambao tayari wanahisi wamelemewa kupita kiasi.
Lakini kweli Nchi ya Kenya haitozwi ushuru wa juu ukilinganisha na mataifa mengine Afrika?
Nchi zinazotoza kodi za juu Afrika

Nchi za Afrika zinazotoza kodi kubwa zaidi zinatofautiana kulingana na aina ya kodi (Mapato, VAT, Ushuru wa Bidhaa), lakini Mauritius, Tunisia, Ushelisheli, Morocco, na Afrika kusini, mara nyingi huonekana kwenye orodha za juu, hasa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Shirika, huku nchi kama Misria zikiongoza kwa kodi kwenye pombe na sigara, lakini hakuna jibu moja, kwani mifumo ya kodi inabadilika na inategemea sekta, kama inavyooneshwa na ripoti za Tax Foundation na OECD.
Kodi ya VAT: Huwa kubwa zaidi, ikiongozwa na Afrika Kusini, Misri, na Kenya.
Kodi ya Mapato: Afrika Kusini na Kenya zina viwango vya juu kwa walio na kipato kikubwa.
Kodi ya Bidhaa Maalum (Excise Duties): Misri, Kenya, na Afrika Kusini zina kodi kubwa kwa pombe, sukari, na sigara.
Kwa mujibu wa Intelpoint, takwimu za mwaka 2024 zinaonyesha kuwa Comoros inaongoza kwa mzigo wa ushuru ukifikia hadi asilimia 50% huku Kenya, Tanzania na Uganda wakiwa katika asilimia ya 30% ya ushuru.