Kampuni ya Buckreef Gold imezidi kuimarisha ushirikiano wake na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia makubaliano ya Uwajibikaji kwa Jamii yenye thamani ya shilingi milioni 600 yanayo lenga kuboresha huduma za afya, elimu, maji na usafi wa mazingira kwa jamii zinazoishi maeneo yanayo zunguka mgodi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, aliipongeza kampuni ya Buckreef Gold kwa namna inavyo tekeleza maendeleo ya jamii kwa nidhamu na kwa kuzingatia sheria. “Buckreef imeonyesha umakini katika kutekeleza wajibu wake kwa kupanga, kutenga bajeti na kutekeleza miradi yake ya Uwajibikaji kwa Jamii kwa kuzingatia matakwa ya serikali. Muhimu zaidi ni jamii kuona matokeo ya wazi na ya kudumu kupitia maendeleo ya shule, vituo vya afya na huduma za maji zinazo boresha maisha ya kila siku.”
Meneja mkuu wa kampuni ya Buckreef Gold, Isaac Bisansaba, amesema kampuni hiyo inaona kuboresha huduma za jamii kama jukumu la msingi ili kuboresha maisha ya wananchi waliozunguka mgodi. “Shughuli zetu zinafanyika ndani ya jamii halisi. Kadri uzalishaji unavyoongezeka, ndivyo wajibu wetu kwa jamii hizo unavyoongezeka. Miradi hii inalenga afya, elimu na maji kwa sababu hapo ndipo athari chanya huhisiwa moja kwa moja na familia.”
Tangu kuanza kwa shughuli za mgodi, jumla ya TZS 1,860,300,000 zimewekezwa katika miradi ya maendeleo ya jamii kote Geita. Miradi mingi kati ya hiyo inaendelea kuhudumia maelfu ya wakazi, kupunguza shinikizo kwa huduma za umma na kuimarisha miundombinu ya kijamii.
Kupitia makubaliano haya mapya ya Uwajibikaji kwa Jamii, Buckreef Gold inaendelea kuonyesha kuwa uchimbaji madini unaowajibika unajengwa juu ya watu, ushirikiano na vitendo vya msingi vinavyoleta matokeo na kutoa thamani ya kudumu kwa jamii za Geita.
Mgodi wa Buckreef Gold unaendeshwa kupitia ubia kati ya TRX Gold Corporation na STAMICO, shirika la madini la serikali ya Tanzania. Muundo huu unaunganisha utaalamu wa kimataifa wa uchimbaji madini na ushiriki wa moja kwa moja wa Serikali, hivyo kuhakikisha uwekezaji wa jamii unaendana na vipaumbele vya kitaifa na mipango ya maendeleo ya wilaya.
#StarTvUpdate