
Vyombo vya habari vya Israel vimetangaza kuwa, Qatar imefanya mazungumzo na Marekani kuhusu kununua nchi hiyo ya Kiarabu ndege za kisasa za kivita za Marekani aina ya F-35.
Juhudi za Qatar za kufufua jaribio lake la miaka mitano la kutaka iuziwe ndege hizo za kivita za kisasa zaidi za Marekani zinafanyika baada ya rais wa nchi hiyo Trump kutangaza mwezi uliopita wa Novemba kwamba, ataiuzia Saudi Arabia ndege hizo zikiwa za kiwango sawa na ilizonazo Israel.
Chaneli ya 12 habari ya Israel, ambayo ndiyo iliyoripoti habari hiyo imesema, utawala wa kizayuni una wasiwasi kuhusu majadiliano hayo kati ya Washington na Doha, ambayo yanaonekana kuwa yako kwenye hatua ya awali.
Ikiwa mazungumzo hayo yatapiga hatua mbele, Qatar itajiunga na Saudi Arabia na Uturuki katika kupigania kumiliki ndege za kivita za F-35, ambazo kwa sasa zinatumiwa na utawala wa kizayuni wa Israel pekee.
Baadhi ya duru za habari zimeripoti kuwa, serikali ya Netanyahu imefanya kampeni kubwa ya kuishawishi Marekani ighairi kukamilisha mauzo hayo kwa Uturuki na Saudia; lakini hata rais wa Marekani Trump naye pia amethibitisha hadharani kuwepo kwa kampeni hizo.
Alipokutana na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman katika Ikulu ya White House mwezi Novemba, Trump aliahidi kwamba Saudi Arabia na Israel zitatendewa na Marekani kama washirika sawa linapokuja suala la kupatiwa ndege za kivita aina ya F-35…/