
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa wa Tehran amesema kuwa, tuna wajibu wa kuwaombea dua Mujahidina wanaojitolea kila kitu chao kwa ajili ya kupigania haki na kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.
Katika khutba za Sala za Ijumaa ya leo iliyosaliwa kwenye Musala wa Imam Khomeini (MA), Hujjatul Islam Sayyid Mohammad Hassan Abu Torabifard ameelezea umuhimu wa miezi mitukufu ya Rajab na Sha’ban na kuitaja kuwa miezi ya ibada na kuimarisha uhusiano wa mtu na Mwenyezi Mungu na kujiandaa kwa ajili ya kuingia kwenye ugeni wa Allah ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na wakati huo huo ametoa mwito kwa umma kwa ujumla, hasa vijana, kushiriki kwa wingi katika ibada mbalimbali ndani ya miezi hiyo mitukufu.
Ameongeza kuwa, miezi ya Rajab na Shaaban ni miezi inayotoa fursa bora ya kunong’ona na Mungu Mwenyezi na kuimarisha imani yake mtu, sambamba na kuilea nafsi kupitia dua na ibada nyinginezo.
Hujjatul Islam Abu Torabi Fard pia amesema: “Sala huimarisha uhusiano baina ya mja na Mwenyezi Mungu na hufungua njia ya kufikia ukamilifu wa kibinadamu.”
Katika sehemu nyingine ya khutba zake, Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema kuwa, miezi ya Rajab na Sha’ban ni fursa muhimu sana katika wakati huu kwani hizi ni enzi ambazo Ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na matatizo mbalimbali. Amesema, hatupaswi kuwasahau watu wa Ghaza na mashujaa wa Palestina. Mujahidina imara wa Yemen na Hizbullah pia wanapaswa kuwa katika fikra na macho yetu muda wote.”
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran pia amezungumzia umuhimu wa kuzingatiwa misingi ya imani, maadili na matendo mema wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.