Mtandao wa al Mayadeen wa Lebanon umeripoti kuwa kundi la wadukuzi wa Iran, Hanzala, limedukua simu ya waziri mkuu wa zamani wa Israel, Naftali Bennett, katika operesheni iliyopelekea kuvujishwa mada nyeti na muhimu.

Kundi la wadukuzi wa Kiirani, Hanzala, limetangaza kwamba limefanikiwa kudukua simu ya waziri mkuu wa zamani wa Israel, Naftali Bennett, kama sehemu ya operesheni ya kielektroniki iliyopewa jiina la “Operesheni Pweza”.

Kwa mujibu wa taarifa za kundi hilo, Hanzala imedukua simu aina ya iPhone 13 ambayo Bennett alikuwa akitumia.

Kundi hilo pia limesema udukuzi huo umepelekea kuvuja masuala nyeti, ikiwa ni pamoja na orodha za mawasiliano zenye nambari za simu za maafisa wakuu wa kisiasa, picha za skrini za mawasiliano ya kibinafsi, na picha za kibinafsi za familia ya Bennett na wanasiasa wa Israel.

Ofisi ya waziri mkuu huyo wa zamani wa Israel imesema kwamba “suala hilo linashughulikiwa na mamlaka za usalama na wataalamu wa usalama wa mtandao,” ikibainisha kwamba kifaa hicho “hakitumiwi kwa sasa.”

Inafaa kuzingatiwa kwamba kundi la “Hanzala” limekuwa likidukua malengo ya kimkakati ya Israel katika mashambulizi ya mtandaoni, na kuibua wasiwasi kuhusu ongezeko la mashambulizi ya mtandaoni dhidii ya maafisa wakuu wa utawala haramu wa Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *