MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Habibu Suluo (pichani) amesema nauli ya Sh 1,000 inayotumika katika mabasi yaendayo haraka ni ya mpito. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Suluo amesema nauli hiyo inayotumika sasa iliridhiwa kuwa Sh 1,000 kwa tangazo la Serikali la Agosti 29, mwaka huu.
Amefafanua kuwa nauli hiyo ni ya mpito wakati Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ukiendelea kukusanya mapendekezo kutoka kwa wadau ili kuja na nauli ya kudumu. “Nauli hizi ni za mpito mpaka pale ambapo Dart atakapowasilisha maoni. Tutaita wadau ili kuona mapendekezo ya Dart baada ya kukaa na watoa huduma kuhusu kiwango sahihi cha nauli.
Tunaposema ya mpito, nauli hii inamtosheleza mtoa huduma asipate hasara wala faida,” alisema. Suluo amesema kiwango hicho cha nauli ya mpito kimewekwa ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania, akisema kinyume chake itakuwa vigumu watu kuja kufanya biashara nchini kutokana na mazingira kutolipa.
Amesema kiwango hicho cha nauli hakihusiani na matukio ya Oktoba 29, mwaka huu, bali matukio ya siku hiyo yalisababisha uharibifu wa miundombinu wakati tangazo la nauli lilikuwa limetolewa tangu Agosti. “Ni kwamba imezoeleka Latra ndiyo hutangaza, lakini Dart walitangaza na sisi tukaridhia, na tangazo likachapishwa kwenye Gazeti la Serikali,” alifafanua. SOMA: Mwendokasi warejea Ubungo kwenda mjini
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Dart, Said Tunda amesema nauli ya Sh 1,000 ndiyo kiwango kinachoweza kumvutia mwekezaji kuleta mabasi, akieleza kuwa jukumu la serikali ni kujenga miundombinu, huku mabasi yakiendeshwa na sekta binafsi. “Tupo kwenye mstari, kwa sababu nia si kuwaumiza wananchi. Baada ya huduma kusimama, watu walikuwa wakilipa kati ya Sh 5,000 hadi Sh 6,000 kwa safari ambayo sasa inalipiwa Sh 1,000,” alisema
