Leo ni Ijumaa tarehe 28 Jamadithani 1447 Hijria sawa na 19 Disemba 2025.
Katika siku kama hii ya leo na miaka 857 iliyopita alifariki dunia Abul-Qasim al-Shatibi, msomi mashuhuri wa Qur’ani aliyekuwa maarufu kwa jina la Imamul Qurra.
Abul-Qasim alizaliwa mwaka 538 Hijiria. Mbali na kuwa mtaalamu mkubwa katika taaluma ya usomaji wa Qur’ani, alikuwa pia mtaalamu wa elimu ya tajweed, tafsiri ya Qur’an, Hadithi, sarufi ya lugha ya Kiarabu na elimu nyinginezo za kipindi hicho.
Licha ya kuwa kipofu lakini alisifika kwa kuwa hodari na alifanikiwa kuhifadhi hadithi nyingi kifuani mwake. Msomi huyo wa Kiislamu ameacha athari kwa vizazi vya baada yake na miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kitabu kiitwacho “al Qasidatus Shatwibiyyah” kilichokusanya masuala yanayohusiana na elimu ya tajweed.

Katika siku kama ya leo miaka 238 iliyopita mwafaka na tarehe 19 Disemba 1787, nchi ya Kiafrika ya Sierra Leone iliunganishwa na Uingereza baada ya kupita miaka 327 tangu ardhi ya nchi hiyo igunduliwe na wazungu.
Sierra Leone “iligunduliwa” na mtalii wa Uhispania na kukoloniwa. Katika miaka ya kukoloniwa kwake na Uhispania, maelfu ya wanaume na wanawake wa Sierra Leone walichukuliwa watumwa na kwenda kuuzwa katika masoko ya Ulaya. Mwenendo huo uliendelea pia baada ya Waingereza kuishinda Uhispania na kuanza ukoloni wa Uingereza nchini humo.
Mwaka 1961 Sierra Leone ilianza kujitawala na kuwa na utawala unaosimamiwa na jeshi, na mwaka 1971 ikawa na utawala wa Jamhuri.

Miaka 145 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, alifariki dunia alimu na mtaalamu wa fasihi wa Kiirani, Mirza Muhammad bin Sulaiman Tankabani.
Mbali na kubobea katika elimu ya fiq’hi, Tankabani pia alikuwa mtaalamu katika fasihi na mshairi mkubwa katika kipindi chake.
Muhammad bin Suleiman ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na “Al Fawaidu fii Usuliddin” na ” Qisasul-Ulama.” Katika kitabu hicho kilichochapishwa mara kadhaa nchini Iran alizungumzia maisha ya maulama wa kabla yake.

Miaka 119 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa kiongozi wa Urusi ya zamani, Leonid Brezhnev katika familia maskini nchini Ukraine.
Mwaka 1931, Leonid Brezhnev alijiunga na kuwa mwanachama wa chama hicho cha Kikomonisti. Brezhnev alitwaa uwaziri mkuu wa Russia na uongozi wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani mwaka 1964 wakati Nikita Khrushchev alipokuwa safarini nje ya nchi.
Mashambulizi dhidi ya Czechoslovakia na kukaliwa kijeshi Afghanistan yalifanyika katika zama zake.

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, Sadeq Ganji mwambata wa Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Lahore Pakistan alishambuliwa kwa risasi na vibaraka wa ubeberu wa kimataifa na kuuawa shahidi.
Kwa karibu miaka minne Ganji alikuwa akitekeleza jukumu lake la kutangaza na kuziarifisha thamani aali za Kiislamu na kupanua uhusiano wa kiutamaduni baina ya wananchi wa Iran na Pakistan.
Sadeq Ganji aliuawa shahidi akiwa amekaribia kurejea hapa nchini baada ya hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na wana utamaduni na shakhsia wa kielimu na kifasihi wa Lahore Pakistan.

Na siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, inayosadifiana na 19 Disemba 1972, kiongozi wa wakati huo wa Uganda, Jenerali Idi Amin Dada, aliwapatia wafanyakazi wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi nchini humo makataa ya siku 12 wakubali kupunguziwa mishahara yao kwa asilimia 40 au waondoke nchini humo.
Zoezi hilo liliwajumuisha karibu wafanyakazi 780 wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashirika mbalimbali nchini Uganda.
